RAIS wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, amefichua kuwa klabu hiyo ilipokea ofa ya dola milioni 2 (takribani Sh bilioni 5) kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wao nyota, Clement Mzize, lakini uongozi uliamua kumbakisha kikosini.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika leo Septemba 7,2025 jijini Dar es salaam, Hersi amesema kulikuwa na ofa nyingi kwa ajili ya Mzize, lakini uongozi uliona bado ana mchango mkubwa kwa kikosi.
“Ofa zilikuwa nyingi sana kwa kijana wetu, lakini Yanga haikuwa na nia mbaya. Tulijua tunachokitaka na kuamua kumbakiza kwa kuwa tunahitaji nguvu yake,” amesema Hersi.
Uamuzi huo umeonyesha msimamo wa klabu hiyo kutokuridhia kuachana na wachezaji wake muhimu wakati huu ikijiandaa kwa mashindano ya ndani na kimataifa.