π Tasnia ya Burudani na Michezo kwa mwaka 2024/2025 imekuwa kwa asilimia 18
π Watumishi 3,353 washiriki SHIMIWI mwaka 2025
π Awahimiza washiriki SHIMIWI kusikiliza kampeni za wagombea na kupiga kura Oktoba 29
π Serikali kujenga Kituo cha Kulea Vipaji Mwanza
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa rai kwa wanamichezo kufanya uchunguzi wa afya zao kwa kuhusisha vipimo vyote muhimu ikiwemo vya moyo, damu na viungo vyote vya mwili ili kuhakikisha usalama wa Afya zao.
Ameliomba Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kuendelea kushirikiana na Taasisi za Afya nchini na kuweka mfumo sahihi wa upimaji wa afya kwa wanamichezo.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo Septemba 7, 2025 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati akifungua rasmi mashindano ya 39 ya SHIMIWI yaliyotanguliwa na maandamano ya watumishi wa umma.
Ametaja masuala mengine muhimu ya kuzingatiwa kwa wanamichezo β Mazoezi ya awali na mbinu nyingine mbalimbali kwa kujenga uimara wa mwili kupitia mazoezi kama vile kukimbia, mazoezi ya nguvu na mazoezi mfano wa hayo. Pia, kuiandaa akili ili kuikabili michezo na mashindano kwa ujumla, wataalamu husema mafanikio huanza katika fikra,β amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kwa kusema Nimejulishwa kwamba, katika michezo ya mwaka wa jana mlisajili watumishi 2,995. Na mwaka huu 2025 mmesajili watumishi 3,353 kushiriki michezo hii ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 12 hongereni sana,β
Pia, ameipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na viongozi wa SHIMIWI kwa kazi kubwa ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza michezo nchini.
Dkt. Biteko pia amewataka waajiri kutekeleza maagizo ya Rais Samia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi wanaoshiriki SHIMIWI huku akiwaeleza watumishi kuwa Rais Samia anawatakia kila la heri katika michezo yao na kuwa yuko tayari kuendelea kushirikiana nao ili kupata mahitaji yao.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa, Tasnia ya Burudani Tanzania ambayo michezo ipo ndani yake imeendelea kukua kwa kasi na kuchangia sehemu muhimu katika Pato la Taifa na kuongeza ajira nchini.
Ametolea mfano kwa mwaka 2022/2023 sekta hiyo imekua kwa asilimia 15 na mwaka 2023/24 kwa asilimia 18. Aidha, uwepo wa watumishi wanaoshiriki SHIMIWU zaidi ya 3,000 Jijini Mwanza umesaidia kutengeneza ajira na kuchangia mzunguko wa fedha.
βNawaomba viongozi muweke mikakati ya kuhakikisha manufaa haya yanawagusa Watanzania wa maeneo yote nchini kwa maslahi mapana ya Taifa kwa ujumla,β amesisitiza Dkt. Biteko.
Halikadhalika amewaasa wachezaji wote kujenga fikra ya kupendana na si kuchukiana baina yao pamoja na kufuata na kuzingatia taratibu zote za michezo.
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amewasihi wanamichezo hao kuhimizana kushiriki kwa amani katika zoezi la kusikiliza kampeni za wagombe na kukumbushana umuhimu wa kupiga kura.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza katika michezo ambapo inajenga Kituo cha Kulea Vipaji katika Chuo cha Michezo Malya.
Pia, amesema shughuli za kampeni mkoani humo zinaendelea vizuri na Oktoba 29, 2025 wananchi watajitokeza kwa wingi kupiga kura.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuruhusu kufanyika kwa mashindano ya SHIMIWI kwa watumishi wa umma kwa miaka mitano mfululizo kwa kuwa yameendelea kuwa na faida kubwa.
β Wizara yetu itaendelea kuhakikisha michezo hii inafanyika kwa haki, sisi kama Wizara tunamshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake na kutoa raslimali fedha ili kukuza sekta ya michezo nchini,β amesema Msigwa.
Ametaja jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta ya michezo ni pamoja na kukamilisha viwanja na shule za michezo katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika michezo kimataifa katika ngazi mbalimbali.
Katika salamu zake za utangulizi, Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa imefanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matokeo chanya.
Awali, Dkt. Biteko ametembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ambapo ameelezwa majukumu na huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mashindano ya Michezo ya 39 ya SHIMIWI kwa mwaka 2025 yanayoongozwa na kaulimbiu βMichezo kwa Watumishi Huongeza Tija Kazini, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu 29 Oktoba 2025 kwa Amani na Utulivu Kazi Iendelee.βyatafikia tamati Septemba 16, 2025.β