Na Mwandishi Wetu, Mara
MGOMBEA wa Urais kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP), Bi. Saumu Rashidi, ameendelea na kampeni zake mkoani Mara , ambako alijinadi kwa wananchi akiahidi kuwa serikali yake itawajengea Watanzania mazingira rafiki ya kiuchumi ili kujaza fedha mifukoni mwao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, Bi. Saumu alisema moja ya malengo makuu ya chama chake ni kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa katika uchumi kwa kupitia uwekezaji, kilimo chenye tija, pamoja na ujasiriamali.
“Tunataka kila Mtanzania aone matunda ya uchumi wa nchi hii. Serikali ya UDP itawafungulia fursa na kuweka mifumo rahisi ya mikopo na masoko ili kila mmoja aweze kunufaika na kazi zake,” alisema Bi. Saumu
Aidha, aliahidi kuwa serikali itakayoundwa na UDP itajikita katika kupunguza gharama za maisha, kuongeza ajira kwa vijana, na kuhakikisha sekta za elimu na afya zinakuwa bora zaidi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, baada ya kumaliza mikutano yake mkoani Mara, mgombea huyo ataendelea na kampeni katika mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, akiwahamasisha wananchi kuunga mkono sera za UDP katika uchaguzi mkuu ujao.