Featured Kitaifa

DKT.SAMIA AAHIDI KUFUFUA ZAO LA CHAI MUFINDI

Written by Alex Sonna

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mafinga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Iringa tarehe 06 Septemba, 2025.

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mafinga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Iringa tarehe 06 Septemba, 2025.

Na Mwandishi Wetu, Iringa

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kufufua na kutafuta masoko ya zao la chai wilayani Mufindi, mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sekta ya kilimo na kuinua kipato cha wananchi.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 6,2025  kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Nyororo, Mufindi, Dkt. Samia amesema kuwa tayari serikali imeunda timu ya tathmini kufuatilia uwekezaji wa sekta binafsi katika zao la chai, ili kubaini iwapo wawekezaji wameshindwa kuliendeleza. Amesema iwapo itabainika hivyo, serikali itaingilia kati kwa kuchukua mashamba na kuyakabidhi kwa vyama vya ushirika vya wakulima.

Aidha, ameahidi kushughulikia malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 2.7 wanazodai wakulima na wafanyakazi wa Kampuni ya Mufindi Tea and Coffee Company, akibainisha kuwa serikali inaendelea na mazungumzo kuhakikisha fedha hizo zinalipwa hivi karibuni.

Katika sekta ya miundombinu, Dkt. Samia amesema kuwa barabara ya Nyororo–Mtwango yenye urefu wa kilomita 40.4 itaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami, sambamba na barabara ya Igowole–Kasanga–Nyigo yenye urefu wa kilomita 54.5. Pia ameahidi kupeleka mashine ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.

Awali, wagombea ubunge kupitia CCM katika majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini walimshukuru Dkt. Samia, kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo wilayani humo. Walitaja miongoni mwa mafanikio hayo kuwa ni utoaji wa zaidi ya shilingi bilioni 40 zilizowezesha ujenzi wa shule mpya 23, ikiwemo sekondari nne na chuo cha ufundi stadi (VETA), hatua iliyopunguza mzigo wa michango kwa wazazi.

Viongozi hao pia wamemshukuru kwa kusogeza huduma ya umeme katika maeneo yote ya wilaya hiyo ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, hatua iliyofanikisha kata zote kupata umeme, huku vijiji na vitongoji vikiwa vimefikiwa kwa zaidi ya asilimia 78. Waliunga mkono pia ruzuku zilizotolewa kwa wakulima wa mahindi na chai, zilizowezesha wananchi kununua mbolea na pembejeo nyingine kwa nusu bei.

About the author

Alex Sonna