Featured Makala

MABADILIKO YA TABIANCHI YAZIWEKA HATARINI DAWA ZA ASILI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma

Kwa miaka mingi dunia imekuwa ikishuhudia matumizi makubwa ya dawa za asili kabla ya kuenea kwa tiba za kisasa ambapo mimea tiba ilikuwa nguzo kuu ya afya katika jamii zetu.

Lakini hivi sasa, mimea hiyo adimu inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na uharibifu wa mazingira ambao umeanza kupunguza kwa kasi mimea ya tiba na hiyo.

Mwaka 2022, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilibainisha kuwa ni dhahiri tiba za asili zina mchango mkubwa katika huduma za afya, ikiwa ni sehemu muhimu ya urithi wa kitamaduni na njia za asili za kutibu magonjwa hususani katika maeneo ya vijijini ambapo huduma za kisasa ni nadra kupatikana.

Katibu wa Umoja wa watengeneza Dawa asili Tanzania (UWADATA), Dkt. Michael Magoti anasema mabadiliko ya tabia ya nchi yamekuwa changamoto kubwa hivyo wanahakikisha wanatumia kampeni ya kata mti panda mti ili kuinusuru mimea tiba iliyoko hatarini.

“Kila kitengo husika kinakuwa na wahusika wa aina fulani ya mimea kwahiyo unakuta ni kampeni kwa mfano, unakuta kila mzalishaji dawa ambaye anatumia mti ambao una hatari ya kupotea anakuwa labda na shamba ambalo anapaswa kupanda miti hiyo kwa wingi kwasababu hatuangalii leo ni kwaajili ya kizazi kijacho,”anasema.

Licha ya jitihada mbalimbali kufanyika ili kunusuru mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabi ya nchi bado kumekuwa na kitendawili kizito juu ya hatma ya miti ya asili kutokana na aina ya miti inayopandwa na hapa Chief wa Mkoa wa Dodoma Mtemi Henri Mzengo anaelezea kuwa miti ya asili ina uhitaji mkubwa si kwa binadamu pekee bali hata kwa ndege ili kuweza kutua na kuweka makazi.

“Ile miti ya zamani Mganga anaifahamu akifika hivi kwamba kuna miti sehemu fulani anakwenda kutafuta tofauti na miti ya sasa hivi ambayo kwao haina nafasi na vilevile madhara mengine ni kwamba hata ndege hawatui kwenye miti ya kisasa kuweza kuweka viota vyao wanahangaika kutafuta miti ya asili ambayo ndiyo inalingana na hali waliyoizoea”,anaeleza.

Aidha, Dkt. Magoti anasema Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki kuwa na mfumo rasmi wa utoaji wa tiba jumuishi ambapo kwasasa inatolewa katika hospitali za rufaa kwenye mikoa 14.

“Tiba jumuishi maana yake unaenda hospitalini Daktari anakusikiliza anakuangalia anajua changamoto yako lakini kwenye kutibiwa anakupa chaguo anakwambia tuna dawa hii ya tiba na zile za kisasa, sasa kazi kwako wewe mteja kuchagua unataka utibiwe na nini,”anasema Dkt. Magoti.

Pia, anaendelea kuwa zipo takribani dawa 26 za tiba asili zinazotolewa katika hospitali hizo za rufaa ambapo tayari zimesajiliwa na baraza zikiwa zimefanyiwa tafiti za awali ili kujilidhisha kama ni safi na salama pamoja na viini tiba ili ziweze kutumika kwa matibabu.

Dkt. Shimo Peter ni Mkurugenzi wa uchunguzi wa bidhaa na mazingira katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia mkuu wa Serikali anasema tangu mwaka 2010 mapaka sasa zaidi ya sampuli 968 za dawa asili zimepimwa.

“Kati ya sampuli hizo au dawa hizo, dawa 140 mpaka sasa hivi zimefanikiwa kusajiliwa na baraza kuu la tiba asili na tiba mbadala na kati ya hizo dawa 26 tayari zitumika katika hospitali zetu za kanda ambapo ukienda hospitali utaweza kupatiwa dawa za asili ambazo zimedhibitishwa na mkemia mkuu wa serikali lakini zimesajiliwa kutumika na zinaendelea kuzalishwa ili kuwezesha kuwa na huduma endelevu, “anasema Dkt. Peter.

Anaongeza kuwa hiyo ni sifa kubwa kwa taifa kwamba kwasasa linauwezo wa kuzalisha na kupima dawa kwaajili ya matumizi ya ndani na hata nje, kwani inawawezesha kuzipima na kumhakikishia mtumiaji kwamba ni salama na zinafaa kwa matumizi ya binadamu.

Chief Mazengo nashauri kuwa ipo haja ya Serikali na wadau mbalimbali wanaopanda miti kuwashirikisha ili kuendeleza miti ya asili ambayo kwasasa ipo kwenye uhatari wa kupotea.

Nao wauzaji wa dawa za tiba asili wanadai kuwa kuja kwa dawa kutoka nje hakuwezi kuathiri biashara hiyo kutokana na uzalishaji wake kuwa wa mimea ya asili.

“Tunapoongelea asili haiwezi kubadilika ila mambo ya kisayansi yataendelea kubadilika, kwanza tupoongelea asili ni mwanzo iliyoanza tangu mababu zetu na mpaka sasa ndo tunaienzi licha ya changamoto mbalimbali kuwepo za watu kuja kuiamini asili yenyewe kwani wengi wanaamini zaidi dawa za kigeni,”wamesema.

Aidha, wameenda mbali zaidi na kubainisha kuwa ipo haja ya watu wa tiba asili kama mgonjwa ana bima imruhusu kuitumia hata kwao watu wa tiba asili kwani wamesajiliwa ili kuweza kuokoa maisha ya watu ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

Baadhi ya tafiti kama zile zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani, WHO, mwaka 2021 na 2022, African Journals Online, AJOL, pamoja na WHO Afro Health Monitor ya mwaka 2021 zimezitaja changamoto za matumizi ya tiba za asili kama vile ukosefu wa uthibitisho wa kisayansi, uelewa mdogo wa jamii kuhusu usalama na ufanisi wake, ukosefu wa mifumo thabiti ya udhibiti, na changamoto za kisheria zinazokwamisha matumizi yake rasmi.

Huku Serikali ya Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikichukua hatua ili kudhibiti matumizi holela ya dawa za asili, ambapo ni pamoja na kudhibiti ubora wa dawa hizo kupitia usajili wa waganga wa tiba asili.

Dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 inaongozwa na nguzo kuu Tatu ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi ikiwa inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi inayothamini, kulinda na kutumia rasimali zake za asili kwa uendelevu, kuhifadhi mazingira na kuwa na ustahimilivu wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hayo.

Kwa kuwa na mikakati madhubuti ya kulinda mifumo ya ikolojia na kukuza ustahimilivu, Tanzania itakuwa ni nchi yenye maisha bora, usawa, na ustawi kwa watu wake na urithi wake wa asili.

Aidha, Dira hiyo imebainisha kuwa tangu mwaka 1980 pamekuwa na ongezeko kubwa la joto ardhini na baharini ambapo makadirio yanaonesha ongezeko la joto la zaidi ya nyuzi joto mbili, huku maeneo ya mashariki yakitarajiwa kuongezeka kwa nyuzi joto moja.

“Kuongezeka kwa joto kunatishia usalama wa
chakula kwa kupunguza uzalishaji wa kilimo na kuleta hatari kubwa za kiafya, ambapo ongezeko la nyuzi joto moja linahusishwa na ongezeko la asilimia 15–29 la maambukizi ya kipindupindu na kuenea kwa magonjwa yanayoambukiza kama
vile homa ya matumbo na kuhara,”imebainisha.

Pia, imeonesha kuwa kuanzia miaka ya 1970 kumekuwa na mabadiliko ya viwango vya mvua ambayo yamesabababisha uhaba wa maji kwa baadhi ya maeneo, ongezeko la mafuriko,
moto wa nyika, kuharibika kwa miundombinu na kuongezeka kwa viumbe na mimea vamizi, pamoja na uharibifu wa matumbawe na bioanuai.

Mabadiliko haya pia yameongeza kuwepo kwa mazalia ya vimelea vya magonjwa kama vile
malaria na homa ya dengue, hivyo bila kuchukua hatua thabiti, mabadiliko ya tabianchi mwaka 2050, na hivyo kuwaingiza watu milioni 2.6 katika umaskini, huku watu milioni 13 wakilazimika kuhama kwenye makazi yao.

Katika kushughulikia changamoto hizo Serikali imefanya jitihada za kuboresha sera na taasisi na kutumia fursa zinazojitokeza kimataifa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, bado kunakosekana urasimishaji wa kutosha wa sera miongoni mwa taasisi za utekelezaji, jambo linalopelekea vikwazo katika
uratibu na utekelezaji kwani wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wamekuwa wahanga wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

About the author

mzalendo