Featured Kitaifa

VIONGOZI AFRIKA MASHARIKI WAAHIDI KUKABILIANA NA UVUVI HARAMU

Written by Alex Sonna
Katika kujenga mshikamano wa kikanda, viongozi wa serikali, wataalamu wa masuala ya bahari na uvuvi, viongozi wa jamii na wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira ya pwani wameweka saini makubaliano ya kihistoria ya kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya Uvuvi Haramu, Usioripotiwa na Usiodhibitiwa katika maji ya Afrika Mashariki.

Makubaliano haya yamefikiwa kupitia Kongamano la Sauti za Buluu lililoandaliwa na Mradi wa Jahazi, hatua ambayo imeweka msingi wa mshikamano wa kikanda katika kushughulikia tatizo linalosababisha hasara ya takribani dola za Kimarekani milioni 415 kila mwaka na kutishia zaidi ya watu milioni 3 wanaotegemea rasilimali za uvuvi kwa maisha yao ya kila siku.

Makubaliano Muhimu

Kongamano hilo limeazimia kutekeleza hatua tano kuu:

  1. Kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia kubadilishana maarifa na usimamizi wa sheria kwa pamoja.
  2. Kuziwezesha jamii za wavuvi ili kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji na kudhibiti uvuvi haramu.
  3. Kuwashirikisha vijana na kuchochea ubunifu wa kiteknolojia katika mapambano dhidi ya uvuvi haramu.
  4. Kuongeza juhudi za elimu na uhamasishaji wa umma kuhusu madhara ya uvuvi haramu.
  5. Kukuza mijadala ya sera endelevu ili kuhakikisha utekelezaji na uwajibikaji.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Michael Mallya, Msemaji wa Mradi wa Jahazi, alisema:

“Ukanda huu wa Pwani ya Afrika Mashariki ni miongoni mwa ikolojia muhimu zaidi za bahari duniani, lakini unakabiliwa na vitendo visivyokubalika vinavyopunguza kiwango cha samaki, kuharibu makazi ya viumbe vya baharini na kuhatarisha usalama wa chakula. Tumeungana hapa kutafuta suluhu ya pamoja; na ili kubadili mwelekeo huu, mshikamano wa kikanda ni jambo la lazima.”

Changamoto na Mbinu za Kiteknolojia

Wadau mbalimbali walieleza changamoto zilizopo na mbinu za kukabiliana nazo.

👉Dkt. Baraka Sekadende kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania, alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti uvuvi wa baruti, kutoka wastani wa milipuko 20–30 kwa siku hadi kutokuwepo kabisa. Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto za rasilimali fedha na nguvu kazi bado ni kikwazo kikubwa.

👉Dkt. Matthew Silas wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) alieleza matumizi ya teknolojia za kisasa kama VMS, AIS na picha za Satelaiti katika kufuatilia vyombo vinavyoshukiwa kufanya uvuvi haramu. Pia alithibitisha kuwa Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Port State Measures (PSMA) unaolenga kuzuia meli zinazojihusisha na uvuvi haramu kutumia bandari za nchi wanachama.

👉Lydia Mgimo kutoka Shirika la Sea Sense alieleza athari za kijamii za uvuvi haramu, zikiwemo kusambaratika kwa familia, wanafunzi kuacha shule na kuongezeka kwa hatari ya usalama wa chakula. Alisisitiza:

“Ukiharibu chanzo cha chakula, unahatarisha mustakabali wa maisha ya jamii nzima za pwani.”

Ubunifu na Ushirikiano wa Kikanda

Kongamano lilisisitiza haja ya suluhu za kudumu kupitia ubunifu na mshikamano wa kikanda. Mashirika kama Blue Ventures, Wildlife Conservation Society (WCS) na Northern Rangelands Trust yaliwasilisha mifano ya ufanisi ikiwemo doria za baharini zinazoongozwa na jamii, miradi ya kusaidiana vifaa, na uhifadhi unaotegemea takwimu.

Sebastiano Lubinda wa Blue Ventures alibainisha changamoto ya kurudia kazi zilezile bila uratibu wa pamoja. Alisema:

“Mashirika hutumia mifumo tofauti ya ukusanyaji wa takwimu kujibu maswali mbalimbali. Kama ukanda, tunapaswa kuoanisha mbinu zetu na kushirikiana katika matumizi ya taarifa.”

Tamko jipya lililotiwa saini limegeuza ahadi za kipekee kuwa msimamo wa pamoja, likiunganisha serikali, mashirika na jamii katika kupanga mikakati na matumizi bora ya rasilimali za bahari.

Wito wa Hatua

Makubaliano haya siyo mwisho wa safari, bali mwanzo wa awamu mpya ya mapambano. Washiriki walikubaliana kuendeleza mshikamano huu kwa njia ya kidijitali, wakionesha kuwa vita dhidi ya uvuvi haramu vinahitaji ushiriki wa sekta zote.

Mallya alihitimisha kwa kusema:

“Tunapoondoka leo, hili ni jambo tunalopaswa kuendelea kulijadili. Tamko hili ni ushahidi wa uelewa wa ukubwa wa changamoto hii na ni ahadi ya pamoja ya kulinda uchumi wa buluu kwa vizazi vijavyo.”

 

 

 

About the author

Alex Sonna