Featured Kitaifa

MAVUNDE AMWAGA AHADI ZA KUIINUA MTUMBA KIMAENDELEO

Written by Alex Sonna

 

Na Alex Sonna,Dodoma

Katika jitihada za kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo ya kweli, Mhe. Anthony Mavunde ameahidi kuibadilisha sura ya Jimbo la Mtumba endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

Akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni Dodoma Mavunde alisema kuwa anahitaji ridhaa ya wananchi wa Jimbo hilo ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi zaidi kwa sababu yeye ni mtumishi wa watu, na anaelewa kwa undani kero na changamoto zinazowakabili.

Amesema moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha Mtumba inageuka kuwa mji wa kisasa unaong’aa, hasa kwa kuzingatia kuwa Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 600.

Ameongeza kuwa Kupitia mpango huu, Mavunde anataka kuona Mtumba inakuwa kitovu cha maendeleo na huduma bora kwa wakazi wake.

Katika sekta ya elimu, Mavunde amekuwa mstari wa mbele. Tayari amejenga shule mbalimbali zikiwemo Shule ya Msingi Chiwondo, Mkoyo na Mahomanyika Sekondari.

Ameahidi kwamba endapo atapata nafasi ya kuwa mbunge, atahakikisha kila eneo lenye upungufu wa shule linapatiwa shule ili watoto wote wapate haki ya msingi ya elimu. Kwa sasa ujenzi wa Shule ya Chawha unaendelea, hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuboresha elimu.

Mavunde pia amegusia changamoto ya michango ya mitihani ya Jumamosi, akisema kuwa atahakikisha michango hiyo inaondolewa ili kupunguza mzigo kwa wazazi.

Aidha, amesema kuwa atahakikisha barabara ya Hombolo – Mayamaya pamoja na barabara nyingine za ndani katika mitaa mbalimbali ambazo ni korofi, zinatengenezwa. Ameahidi kununua greda maalum litakalotumika kuimarisha barabara hizo mara kwa mara.

Katika sekta ya maji, Mavunde amesema kuwa uwezo wa kuzalisha maji jijini Dodoma umefikia lita milioni 47 kwa siku na kueleza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kata zote ikiwemo Hombolo, Ihumwa, na Mahomanyika zinapata huduma ya maji safi na salama.

Ameahidi kuwa huduma hiyo itatolewa bure kwa baadhi ya maeneo yenye uhitaji mkubwa kama njia ya kupunguza gharama kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Mtumba wamezungumza na Mzalendo Blog kuwa Mavunde anaonekana kuwa na maono makubwa kwa Jimbo lake, akilenga kuboresha miundombinu, huduma za kijamii na uchumi wa wananchi.

About the author

Alex Sonna