Featured

WANANCHI TUNZENI BARABARA KWA KUZIFANYIA USAFI: MHANDISI MATIVILA

Written by Alex Sonna

Ukerewe, Mwanza

Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amewataka wananchi kuhakikisha wanazitunza barabara kwa kuzifanyia usafi ili zidumu kwa muda mrefu.

Mhandisi Mativila ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara zinazosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Amesema wananchi wanatakiwa kuzifanyia usafi barabara hizo mara kwa mara badala ya kuzigeuza kama dampo la kutupitia takataka.

Ameongeza kusema kwamba barabara hizo zikitunzwa vizuri zitachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, ikiwemo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuongeza ajira kutokana na kupitika kipindi chote cha mwaka.

Amesema serikali inaendelea kuimarisha mtandao wa barabara nchini kwa kujenga barabara mpya na kuzifanyia matengenezo zilizopo.

Naye, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Makori Kisare, akitoa taarifa ya matengenezo ya barabara za lami za RTC – Sungura yenye urefu wa Km 0.321 na barabara ya Pump House Km 0.299 katika mji wa Nansio, amesema barabara hizo zimegharimu zaidi ya Sh. Mil. 470 kutoka mfuko wa jimbo.

Amesema barabara hizo zimeboreshwa kutoka kiwango cha changarawe kwenda kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2023/2024 na ametaja kazi zilizofanyika kwenye mradi huo kuwa ni pamoja na uwekaji wa taa 21 za barabarani pande zote za barabara, ukarabati wa ujenzi wa mitaro ya maji na ujenzi wa kalvati kwa ajili ya kutoa maji barabarani.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubiagai akizungumzia hali ya miundombinu ya barabara za wilaya hiyo amesema uamuzi wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Rais, anayesimamia miundombinu kufika wilayani humo kwa ajili ya kujionea hali ya miundombinu ilivyo inaleta matumaini makubwa kwa wananchi na wadau wa vyombo vya usafirishaji.

Amesema kilio cha muda mrefu cha wananchi wa wilaya hiyo inayoundwa na visiwa 38 ni barabara, ambazo baadhi yake zimekuwa hazipitiki kutokana na kuharibika jambo ambalo limekuwa ni kero na kusababisha kupanda kwa nauli.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Nansio, wameipongeza serikali kwa matengenezo ya barabara hizo zenye jumla ya urefu wa Km 0.62, kwani awali hali ya upitikaji wa barabara hizo haikuwa rafiki hasa kipindi cha mvua.

Mradi wa barabara za RTC – Sungura na Pump House umetekelezwa na Mkandarasi Deep Construction Ltd ya Morogoro chini ya usimamizi wa TARURA wilayani Ukerewe, mradi huo umetekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja.

About the author

Alex Sonna