Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa BMH, Jeremia Mwakyoma, ujenzi huo unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 30.4.
Aidha, Dk. Mpango atazindua rasmi mradi wa upanuzi wa Kituo cha Upandikizaji Figo, wenye thamani ya shilingi bilioni 1.7.
Pia , Makamu wa Rais atashuhudia hatua ya Serikali ya Tanzania kupitia BMH kuwa mwenyeji wa ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uti wa Mgongo (bone marrow transplant) na Sayansi ya Magonjwa ya Damu, chini ya ridhaa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa wananchi wote wanakaribishwa kushiriki katika hafla hiyo.