MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele,akiwaongoza Maafisa ,Askari na Vijana kupanda miti katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT, pamoja na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 61 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964,
Na.Alex Sonna-CHAMWINO
KATIKA kuadhimisha miaka 61 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tangu kuasisiwa kwake Septemba 1, 1964, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, ameongoza Maafisa ,Askari na Vijana kupanda miti ya katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT, pamoja na kuchangia damu katika Hospitali ya Uhuru, Chamwino jijini Dodoma.
Akizungumza katika maadhimisho hayo leo Septemba 1,2025 , Meja Jenerali Mabele ametoa wito kwa taasisi mbalimbali nchini kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma hiyo muhimu.
Amesema kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, vikosi vyote vya JWTZ vimeadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kupanda miti, kufanya usafi na kuchangia damu katika maeneo yanayowazunguka.
“Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania ni mali ya wananchi, hivyo katika sherehe hizi ni lazima turudi kwa jamii. Sisi JKT tumeona tujitolee damu kwa wahitaji, tukitambua uhitaji ni mkubwa,” amesema Meja Jenerali Mabele.
Ameongeza kuwa vijana wa JKT wamejitokeza kuchangia damu kutokana na kutambua uhitaji mkubwa uliopo hospitalini. Aidha, amewaongoza Maafisa Askari na Vijana kupanda miti ya kumbukumbu katika maeneo yanayozunguka Makao Makuu ya JKT.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kambi Makao Makuu ya JKT, Kanali Geofrey Mvula, amesema pamoja na kupanda miti na kuchangia damu, pia elimu imetolewa kwa Maafisa, Askari Vijana kuhusu umuhimu wa kuchangia damu, jambo lililowahamasisha wengi kushiriki.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Uhuru, Devotha Rweyemamu, ameushukuru uongozi wa JKT kwa hatua hiyo ya kuja kujitolea damu katika hospitali yetu kwani itaweza kusaidia wagonjwa mbalimbali waliopo hospitali hapo.
“Hospitali hii ipo barabarani, hivyo inapokea wagonjwa wengi wa ajali na huduma nyingine zinazohitaji damu kwa wingi. Hivyo msaada huu ni muhimu sana kwa wagonjwa wetu,” amesema Devotha.
Aidha ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano wa JKT wa kufika katika hospitali hiyo kutoa msaada wa kutoa damu Salama.