Featured Kitaifa

WADAU WATAKIWA KUTEKELEZA UTOAJI WA HUDUMA ZA USTAWI KWA VITENDO

Written by Alex Sonna

Na WMJJWM-Dar Es Salaam

Wizara, Taasisi na Mashirika binafsi, zimetakiwa kutekeleza utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii kwa vitendo ili kuwa na jamii yenye uwezo wa ustahimilivu na yenye mchango wa kuleta maendeleo kwa mtu, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa mkoani Dar Es Salaam Agosti 30, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Kilele cha Wiki ya Ustawi wa Jamii kilichofanyika katika Viwanja vya Ustawi wa Jamii Kijitonyama.

Dkt. Jingu amesema uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini umeendelea kuongezeka kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kutokana na mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha yakiwemo ya uchumi, siasa, jamii.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, wadau wa maendeleo na mashirika ya hiari inashughulikia changamoto zinazowakabili makundi maalum na jamii kwa ujumla.

“Natoa rai kwa wazazi/walezi na watanzania kwa ujumla kulinda haki na Ustawi wa Jamii kwa watoto wetu ili kuilinda nguvu kazi ya Taifa kwa maisha ya baadae. Kwani ulinzi na usalama wa watoto wetu ni jukumu letu sote.” amesema Dkt. Jingu

Aidha ameziasa Mamlaka za Wilaya na Mikoa kuhakikisha zinatenga Bajeti ya Huduma za Ustawi wa Jamii na kusimamia utekelezaji wake kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma hizo kwa wananchi huku akisema Wizara kwa kushirikiana na wadau wataendelea kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi/walezi na jamii kwa ujumla ili kuimarisha mfumo wa malezi kwa kulinda nguvu kazi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la UNICEF Elke Wisch akitoa salamu zake wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma Bora kwa watoto kwenye Vituo vya Kulelea Watoto mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama zinatolewa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Children in Crossfire (CIC) Craig Fera akitoa salamu zake wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo amesema huduma za ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika jamii hasa katika hatua za mwanzo za binadamu za ukuaji wa watoto hivyo sekta ya Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana ni Msingi katika Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Mwakilishi wa Baraza la Wazee Mzee Ramadhan Matimbwa akitoa salamu zake wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Ustawi wa Jamii amesema Baraza hilo linaishukuru Serikali na Wadau katika utoaji wa huduma kwa wazee katika kuimarisha ulinzi na ustawi wao.

Wiki ya Ustawi wa Jamii imefanyika kwa Siku Sita katika Viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar Es Salaam kuanzia Agosti 25- 30, 2025 ikiongozwa na Kaulimbiu isemayo: “Pata Msaada wa Kisaikolojia; Imarisha Afya ya Akili”.

About the author

Alex Sonna