Featured Kitaifa

DKT.ASHA-ROSE  MIGIRO AWASIHI WANACHAMA KUUNGANA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Written by Alex Sonna

Na Meleka Kulwa -Dodoma

KATIBU Mkuu mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt, Asha-Rose Migiro, amemshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo muhimu ndani ya chama.

Akizungumza mara baada ya mapokezi hayo katika viwanja vya Makao makuu ya Chama cha Mapinduzi CCM (whitehouse) Dodoma Dkt, Migiro amesema uteuzi huo ni heshima kubwa na dhamana ya kuendeleza misingi ya uongozi wa chama, huku akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi, bidii, na uaminifu mkubwa.

“Ninatoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini na kunipa jukumu hili ni heshima kubwa kwangu, na naahidi kulitumikia chama chetu kwa moyo wangu wote,” amesema Dkt. Migiro.

Aidha amewataka wanachama hao kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotaraji kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Pmoja na haya amewashukuru wanachama wa CCM kwa mapokezi mazuri aliyoyapata, akisema kuwa ni ishara ya mshikamano, upendo na ushindi uliopo ndani ya chama hicho tawala.

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt, Emmanuel Nchimbi, amempongeza Dkt. Migiro kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo, akimtaja kuwa ni kiongozi mahiri, mwenye uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma na siasa, ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

Dkt. Nchimbi pia amemshukuru Mwenyekiti wa CCM kwa imani aliyomuonyesha katika kipindi chote alicholitumikia chama akiwa Katibu Mkuu, na akawashukuru wanachama wa CCM kwa ushirikiano waliompa.

“Nilijiunga na chama hiki nikiwa kijana mdogo nimejifunza mengi, nimetumikia katika nyadhifa mbalimbali, na naondoka nikiwa na imani kuwa chama kiko katika mikono salama,” alisema Dkt. Nchimbi.

Hata hivyo Kwa mara ya kwanza katika historia, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeandika historia baada ya kumteua Dkt Asha-Rose Migiro kuwa Katibu Mkuu wake wa kwanza mwanamke tangu kianzishwe mwaka 1977 baada ya kuviunganisha vyama vya ukombozi vya TANU kwa upande wa Tanzania Bara na Afro-Shiraz kwa upande wa Zanzibar.

Katika uhai wake wa miaka 48, CCM imekuwa ikiongozwa na Makatibu Wakuu wanaume kuanzia Mzee Pius Msekwa hadi Dkt Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 29.

Dkt Migiro ni mwanamama mwanazuoni aliyebahatika kupata uzoefu wa kufanya kazi za kimataifa alipoteuliwa na Katibu Mkuu wa nane wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chombo hicho cha kimataifa.

Ban Ki-Moon aliongoza Umoja wa Mataifa kwa miaka minane kuanzia 2007 hadi 2016 alipomaliza muda wake.

Kabla ya kuingia kwenye uongozi wa serikali pale alipoteuliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dkt Migiro alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alizidi kupata uzoefu zaidi katika diplomasia ya kimataifa baada ya Rais hayati John Pombe Joseph Magufuli kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, ambayo ni mtawala wa kikoloni wa iliyokuwa Tanganyika baada ya kumalizika kwa Vita ya Kwanza ya Dunia hadi kupatikana kwa uhuru Desemba 9, 1961.

About the author

Alex Sonna