Featured Kitaifa

MRADI WA TACTIC WALETA MANDHARI MPYA DODOMA

Written by Alex Sonna

Jiji la Dodoma linaendelea kubadilika kwa kasi kupitia utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), mradi unaoonekana kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya mandhari na maisha ya wananchi wa mji huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Dkt. Fredrick Sagamiko, amesema mradi huo umeleta suluhisho la changamoto za muda mrefu hususan katika nyanja za miundombinu na biashara. Barabara mpya zenye urefu wa kilomita 10.19 zinazojengwa kupitia mradi huo zimetajwa kuwa nguzo muhimu ya kufungua upya maeneo ya huduma na kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Aidha, ujenzi wa Soko la Majengo unatajwa kuwa mkombozi wa wafanyabiashara ambao kwa muda mrefu walifanya shughuli zao katika mazingira magumu. Soko hilo jipya litakuwa na huduma za kisasa ikiwemo maegesho ya magari na nafasi kwa wafanyabiashara 875, hali inayotarajiwa kuongeza mzunguko wa biashara na kukuza uchumi wa wananchi.

“Ujio wa mradi huu ni ukombozi tosha kwa wananchi. Soko la majengo halikuwa linaendana na hadhi ya Dodoma, lakini sasa tunapata sura mpya ya mji,” alisema Dkt. Sagamiko.

Wananchi pia wameonyesha matumaini makubwa kutokana na mradi huo. Bi. Rozy Mtundu, mfanyabiashara katika Soko la Majengo, alisema ujenzi wa soko jipya utawasaidia kufanya biashara kwa heshima na hadhi, huku Bw. Laurent Munish akiipongeza serikali kwa kuondoa kero za muda mrefu zilizowakwamisha wafanyabiashara.

Faida za mradi huo hazijabaki sokoni pekee. Katika eneo la Ilazo ujenzi wa mitaro ya maji unaendelea, Nzuguni inapata stendi mpya ya daladala pamoja na mnada wa kisasa, huku wakazi wa Mkalama wakinufaika na barabara mpya inayoongeza thamani ya maeneo yao na kurahisisha huduma za usafiri.

Kwa ujumla, mradi wa TACTIC unaonekana si tu kuboresha miundombinu bali pia kuandika upya sura ya jiji kuu la Tanzania, likielekea kwenye hadhi yake ya kuwa makao makuu ya nchi kwa miundombinu ya kisasa na uchumi shirikishi.

About the author

Alex Sonna