Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,akizungumza leo Agosti 24,2025 jijini Dodoma katika Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 lililoandaliwa na Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania.
…..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameeleza umuhimu wa kuhakikisha Taifa linaendelea kudumu katika misingi imara iliyowekwa na waasisi wake, ambayo ni haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano wa viongozi wa dini ni nguzo muhimu katika kudumisha misingi hiyo.
Akizungumza leo katika Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 lililoandaliwa na Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Rais Dkt. Samia amesema kuwa uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia inayopaswa kwenda sambamba na kulinda utulivu wa taifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema Rais Dkt. Samia akizungumza katika kongamano hilo ametaka “Kudumisha amani ni utamaduni wetu tuliojijengea katika demokrasia ya uchaguzi. Tuendeleze utamaduni huu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu,” amesema Rais Dkt. Samia. Ameongeza kuwa kipindi cha uchaguzi huongeza joto la kisiasa, lakini amani itaendelea kudumu ikiwa viongozi wa dini, kijamii na kisiasa watashirikiana kuhubiri amani na mshikamano kwa kuepusha migongano isiyo ya lazima.
Akizungumzia nafasi ya wadau mbalimbali katika kudumisha amani wakati wa uchaguzi, Rais Dkt. Samia amewataka wanasiasa kuepuka lugha za uchochezi katika kampeni na badala yake kujikita katika sera na hoja.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Rais Dkt. Samia pia amekumbusha nafasi muhimu ya vyombo vya habari katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
“Waandishi wa habari ni kundi muhimu kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu. Kalamu zao zinaweza ama kudumisha au kuhatarisha amani ya nchi yetu,” amesema Rais Dkt. Samia.
Hata hivyo Amesisitiza kuwa mchango wa Serikali katika kukuza sekta ya habari nchini, hatua inayolenga kuongeza uwazi na uhuru wa kujieleza.
Rais Dkt. Samia amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi siku ya Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba, 2025, akibainisha kuwa kushiriki kupiga kura ni wajibu wa kikatiba na kizalendo unaojenga mustakabali wa taifa.