Featured

DKT.MPANGO ATAKA MASHIRIKA YA UMMA KUJITANUA ZAIDI NJE YA NCHI KATIKA ZAMA ZA UTANDAWAZI

Written by Alex Sonna

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

………….

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema zama za utandawazi zinayataka Mashirika ya Umma, Taasisi na Wakala za Serikali kuendelea kutoa huduma mbalimbali hata nje ya mipaka ya nchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Aidha Amewahimiza Wenyeviti wa bodi na Watendaji wakuu wa Mashirika ya umma, kuhakikisha wanatoa uongozi na mwelekeo wa Mashirika ili yaweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi, ambao ndio wana hisa wake wakubwa. 

Amesema ni muhimu kujenga ushirikiano ili kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi. Ameongeza kwamba Taasisi na Mashirika ya Umma hayana budi kuwa daraja baina ya Taifa na dunia ili kuhakikisha Tanzania inatambulika kimataifa, kama nchi yenye mazingira bora ya biashara na uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji nje ya mipaka. Pia amesema ni vema kuimarisha ubora wa huduma pamoja na kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya mabadiliko.  

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo ambazo ni nyenzo muhimu katika kufikia azma ya kujenga mazingira ya ushindani. Ametoa wito kwa Taasisi na Mashirika ya umma kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha, kudhibiti manunuzi na kuimarisha usimamizi wa mikataba pamoja na kusimamia vema rasilimali watu.

Vilevile, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kujenga ushirikiano wa kitaasisi kati ya Mashirika ya Nchini na yale ya Kimataifa, ili kunufaika na masoko, teknolojia, tafiti na hata utamaduni wa kufanya kazi.

Pia amesema ili kufikia malengo ni vema kuongeza bidii na weledi katika kazi ikiwa ni pamoja na ubunifu na ustadi katika uzalishaji na utoaji huduma mbalimbali.

Amewasihi Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu kusimamia weledi katika kazi na kuimarisha suala la utafiti kwa maendeleo ya nchi.

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza maelekezo mahsusi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza utegemezi kwa Serikali, na pia kuweza kuchangia ipasavyo kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.  

Makamu wa Rais amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, ni muhimu kuzingatia kuwa Mashirika ya umma, Taasisi na Wakala za Serikali zinapaswa kuhakikisha zinatekeleza kwa ufanisi wajibu wake na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake. Ameongeza kwamba kwa kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwake, Mashirika ya umma yanawajibika kuhakikisha yanatoa huduma bora kwa jamii na kuendelea kuwa na ushindani wa kibiashara. 

Amesema usimamizi madhubuti wa Taasisi na Mashirika ya umma ni miongoni mwa ajenda kuu za Serikali, ili kuhakikisha uwekezaji uliofanyika unazalisha tija na thamani kwa Taifa. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema Mashirika na Taasisi za Umma yana mchango mkubwa unaotarajiwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Amesema mchango huo unatarajiwa katika kuliongoza Taifa katika ujenzi wa miundombinu ya uchumi, kuiwezesha Sekta binafsi vizuri, utafiti sayansi na teknolojia, rasilimali watu pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Awali akitoa taarifa kuhusu kikao kazi hicho, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema mageuzi makubwa yamefanyika ambapo thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika ya Umma umeongezeka kwa asilimia 82 kutoka trilioni 65 mwaka 2020 hadi trilioni 86 mwaka 2025.

Amesema mafanikio hayo ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliyofanywa katika sekta za kimkakati kama nishati na miundombinu. Ameongeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea na kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya umma na kufanya maboresho ya kiutendaji ili kuhakikisha idadi ya Mashirika yanayochangia katika mfuko mkuu wa serikali yanaongezeka.

Aidha kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la Taasisi ambazo zinapunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu pamoja na uimarishaji wa huduma zinazoenda kwa wateja na jamii nzima. 

Kikao kazi hicho cha Siku tatu kinawashirikisha Viongozi zaidi ya Mia Sita Hamsini kutoka Taasisi, Mashirika na Wakala wa Serikali. Kauli mbiu ya Kikao hicho ni “Kujenga Ushirikiano Endelevu katika Mazingira ya Ushindani wa Kimataifa – Wajibu wa Mashirika ya Umma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kufungua Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Viongozi mbalimbali wakati alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kufungua Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba (NHC) Hamad Abdallah kuhusu miradi mbalimbali ya makzi ya bei nafuu, wakati akikagua mabanda ya maonesho katika katika ufunguzi wa Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki katika ufunguzi wa Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati akifungua Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mfumo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma wakati wa ufunguzi wa Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi tuzo ya mshindi wa kwanza kwa Mashirika ya Serikali yanayofanya biashara kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wa ufunguzi wa Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo na zawadi maalum iliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina wakati wa ufunguzi wa Kikao-kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) leo tarehe 24 Agosti 2025. Anayekabidhi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo.

About the author

Alex Sonna