Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (Dodoma Press Club) wamepatiwa mafunzo ya usalama wa kimwili, kidijitali na afya ya akili, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujilinda binafsi katika mazingira ya kazi.
Mafunzo hayo yalifanyika Agosti 16, 2025, yakiongozwa na Mkufunzi wa Usalama na Ulinzi, Okuly Julius, ambaye pia ni mwandishi wa habari. Okuly alipata mafunzo hayo kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kisha kupewa jukumu la kuwajengea uwezo waandishi wenzake katika mikoa.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Okuly amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari muda wote kwani usalama huanzia kwa mwandishi mwenyewe.
“Ni muhimu kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya mashambulizi ya kimtandao kwa kuhakikisha viunganishi vinavyopokelewa vinathibitishwa kabla ya kubofya, kutumia nywila imara na kuweka uthibitishaji wa hatua mbili. Waandishi wanapaswa kuwa makini zaidi hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kipindi ambacho mara nyingi huambatana na vitisho, ukatili na hata kukamatwa kiholela,” alisema Okuly.
Ameongeza kuwa ni vyema waandishi kutoa taarifa kwa watu wa karibu au wenzao wanapokwenda kwenye kazi, ili kuepuka hatari zinazoweza kutokea endapo watapatwa na matatizo wakiwa peke yao.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Bahati Msanjila (Crown Media), Saida Issa (Gazeti la Zanzibar Leo), Rhoda Simba (Channel Ten), Gideon Gregory (Jambo FM) na Joyce Kasiki (Gazeti la Majira), walisema yamewajengea uwezo mkubwa na sasa wanafahamu mbinu bora za kufanya kazi kwa usalama.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “Empowering Journalists for Informed Community” (Kuwawezesha Waandishi wa Habari ili Jamii Iweze Kupata Taarifa Sahihi) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC). Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa International Media Support (IMS), Union of Tanzania Press Clubs (UTPC) na JamiiAfrica.