Featured Kitaifa

MSD YAIMARISHA USAMBAZAJI WA DAWA NCHINI

Written by Alex Sonna

  

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa,akisisitiza jambo kwa  Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa (hayupo pichani) wakati akizungumzia kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.

Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

SERIKALI  imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini , hatua ambayo imeongeza uwezo wa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamesemwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa,wakati akizungumza na  Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.
Msigwa, amesema kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“MSD imekuwa mhimili muhimu katika utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kusogeza huduma bora za afya kwa wananchi kwa kuhakikisha usambazaji wa dawa na vifaa tiba unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi,” amesema Msigwa.

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, idadi ya vituo vinavyohudumiwa na MSD imeongezeka kutoka 7,095 mwaka 2021/22 hadi kufikia 8,776 mwaka 2024/25,idadi hiyo sawa na ongezeko la vituo 1,681.

Msigwa ameeleza kuwa vituo hivyo vinahudumiwa kupitia kanda 10 za MSD zilizopo katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.

 Serikali imeongeza thamani ya bidhaa za afya zinazozalishwa na viwanda vya ndani. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, bidhaa za afya za thamani ya shilingi billioni 15.9 zilinunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani. Thamani hii imeendelea kuongezeka na kufikia shilingi billioni 98.72 kwa mwaka wa fedha 2024/25.
“Kupitia hatua hii, Serikali imepunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, kulinda ajira za Watanzania, na kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni,” ameongeza Msigwa.
Katika kuboresha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, MSD imenunua na kusambaza vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 429.2 katika vituo vya afya nchini. Baadhi ya vifaa hivyo ni pamoja na mashine za usingizi, mashine za CT-Scan, MRI 3T, Ultrasound, pamoja na digital X-Ray.
Hatua hizo ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya, bila kujali mahali alipo.
Aidha Msigwa, amesema kuwa serikali  imetoa kiasi cha sh bilioni 642.1 kwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo mbalimbali hapa nchini. 

Pia, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, serikali imetoa Sh. bilioni 196.3, kati ya bajeti ya Sh. bilioni 200, iliyokuwa imewekwa, sawa na asilimia 98, fedha hizi zimetumika kununua dawa na vifaa tiba.

 Msigwa amesema, serikali imevunja rekodi kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya dawa na vifaa tiba, tangu kuanzishwa kwa MSD  mwaka 1994.

“Tumeandika rekodi ya kutoa fedha nyingi za vifaa tiba na dawa kuliko wakati mwingine wowote. Tangu kuanzishwa kwa MSD, hatujawahi kufikisha asilimia 98 ya bajeti iliyowekwa,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Mavere Tukai,amesema katika juhudi za kuimarisha usalama wa wagonjwa na kudhibiti uingiaji wa dawa bandia sokoni, MSD imetangaza mpango wa kuanzisha mfumo maalum wa kidijitali utakaowezesha ufuatiliaji wa dawa kuanzia kiwandani hadi inatapomfikia mgonjwa.
Amesema kuwa  mfumo huo unalenga kuhakikisha kuwa kila dawa inayosambazwa kupitia mnyororo rasmi wa MSD inakuwa salama na bora kwa matumizi ya binadamu.
“Tunaenda kuanzisha mfumo wa kufuatilia ubora wa dawa kutoka zinapotengenezwa hadi zinapomfikia mgonjwa. Hii ni hatua muhimu ya kuzuia uwezekano wa dawa bandia kuingia kwenye mnyororo wa usambazaji,” amesema 

Ameongeza kuwa mfumo huo utakuwa chachu ya mageuzi makubwa katika udhibiti wa bidhaa za afya nchini kwa kuwa utaongeza uwazi, uwajibikaji na usalama kwa watumiaji wa dawa.

“Lengo letu ni kuhakikisha dawa zote zinazotolewa kupitia MSD ni bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa,” amesisitiza 

About the author

Alex Sonna