Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Shirika la WILDAF limeanza kuwanoa wagombea wanawake nchini na kuwapa mikakati ya kampeni ili waweze kushinda kwenye uchaguzi mkuu na kuongeza wanawake viongozi.
Mafunzo hayo yanayofanyika wiki hii, yanawajumuisha wanawake 200 wakiwemo 100 kisiwani Zanzibar na Pemba pamoja na 100 jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa WILDAF Wakili Anna Kulaya amesema hayo wakati akitoa maelezo juu ya mafunzo hayo jijini Dar es Salaam ambapo alisema wagombea wanawake wanajengewa uwezo wa namna ya kufanya kampeni, kuongea na hadhira, usalama wao binafsi na usalama wa taarifa na wa kidijitali.
Malunde 1 blog imefanikiwa kuongea na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo jijini Dar es Salaam ambapo mgombea wa tiketi ya CCM kwa nafasi ya Udiwani katika Kata ya Ndugumbi Bi. Amina Zuberi Mtemvu amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kujua vitu vinavyotakiwa na visivyotakiwa wakati wa kampeni.
“Mafunzo haya yametujengea kujiamini wakati wa kuomba kura”, amesema Mtemvu.
Kwa upande wake, Saida Kupela mgombea udiwani wa kata ya Vingunguti kwa tiketi ya ACT amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuwa kiongozi wa mabadiliko anaefikilia mafanikio badala ya kuwa mtawala.
“Mafunzo haya yamenipa ujasiri kwamba ninaweza iwapo nitajiamini,” amesema Kupela.
Naye Salma Kalokola mgombea udiwani kwa tiketi ya CUF katika kata ya kivule amewashukuru WILDAF na kusema kuwa mafunzo haya yamemsaidia kujua namna ya kushiriki uchaguzi mkuu kama mwanamke na kuwa jasiri zaidi.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo Bi Rose Ngunangwa amewataka wanawake hao kuhakikisha kwamba wanakuwa matarishi wa amani na kutoa matumaini kwa wapiga kura wakati wa kampeni zao ili waweze kupita.
Vilevile, amewaasa wagombea hao kulinda sana taarifa zao za muhimu yakiwemo majina matatu na simu zao ili zisitumike vibaya kuzima ndoto zao za Uongozi.
Mafunzo haya yanafanywa na WILDAF kupitia mradi wa Irish Aid Wanawake Sasa unaofadhiliwa na Serikali ya Ireland ambapo pamoja na mengineyo wagombea wanafundishwa namna ya kukabiliana na ukatili mtandaoni, usalama wa taarifa, usalama wao binafsi na wa kidijitali.
Vilevile mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wagombea namna ya kujenga amani na kutatua migogoro ambapo yamejumisha wagombea kutoka vyama vya CCM, ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi CHAUMA na CUF.