Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
HATIMA ya vigogo wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) akiwemo katibu mkuu wa chama hicho Joseph Misalaba itajulikana Septemba 9 mwaka huu ambapo Mahakama ya Wilaya ya Dodoma itakapotoa uamuzi mdogo wa mapingamizi ya awali.
Wanachama watatu wa CWT, Mateseko Bulugu, Elina Pallangyo na Masangu Ntingi
wameiomba Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kutoa idhini ya kufungua shauri la jinai kwa walalamikiwa wanne ambao ni dhidi ya Joseph Misalaba (Katibu Mkuu wa CWT), Nashon Kududu (Mhazini wa CWT), Linus Nyalusi na Kampuni ya Pyrire and Industries kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za chama hicho.
Katika shauri hilo lililombele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Zabibu Mpangule jana lilikuwa kwa hatua ya kusikiliza hoja za mapingamizi ya awali ambapo Wakili Fred Peter Kalonga anayewatete walalamikaji aliiambia mahakama kuwa wateja wake wameomba Mahakama iridhie waombaji kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya walalamikiwa hao kwa kuzingatia kifungu cha 99(1), cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Pia kwamba Mahakama iridhie kupitisha hati ya mashtaka kama msingi wa maombi haya kwa ajili ya kuzingatiwa na kutoa unafuu mwingine wowote ambao Mahakama itaona unafaa kutolewa.
Kwa upande wa wakili wa wajibu maombi, wakili Miriam Mbangati ameiomba mahakama itupilie mbali shauri hilo kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa walalamikaji hawajapata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye ndio mwenye wajibu wa kisheria wa kusimamia mashauri ya jinai.
Akitoa uamuzi wa mahakama baada ya kusikiliza hoja za upande zote, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Zabibu aliiahirisha shauri hilo namba 15805/2025 hadi Septemba 9 mwaka huu ambapo atatoa uamuzi wa mapingamizi, uamuzi ambao utatoa mwelekeo wa kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya walalamikiwa hao au la.
Akizungumza nje ya mahakama mmoja wa wanachama wa CWT, Juma Suleiman alisema wanaimani na mahakama kwamba itatoa uamuzi ambao utasaidia kuokoa mali za chama.