KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu,akizungumza katika kongamano la pili la siku ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu,(hayupo pichani) akizungumza katika kongamano la pili la siku ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
SEHEMU ya washiriki wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu,(hayupo pichani) akizungumza katika kongamano la pili la siku ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kutekeleza miradi ya uzalishaji iliyo endelevu badala ya kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika kongamano la pili la siku ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Dkt. Jingu amesema mabadiliko ya sera za nchi zimeathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa ufadhili wa moja kwa moja kwa mashirika hayo, hivyo kuna haja ya kujiandaa mapema kwa kutumia vyanzo mbadala.
“Ni muhimu mashirika haya kuanza kufikiria miradi ya ndani inayotumia rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao ili kuendeleza huduma wanazozitoa kwa jamii,” amesema Dkt. Jingu.
Aidha ameongeza kuwa wakati umefika kwa NGOs kujitathmini na kubadili mikakati ya utekelezaji wa miradi, kwa kuzingatia hali ya kiuchumi na kisera duniani.
Hata hivyo Dkt. Jingu, amesema kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini yanapaswa kuwa mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema mashirika hayo yanabeba dhamana kubwa ya kuleta ustawi kwa jamii, hivyo ni muhimu yakahakikisha miradi inayotekelezwa inalenga kuleta tija na kuendeleza maisha ya wananchi, hususan katika maeneo yaliyo katika mazingira magumu.
Dkt. Jingu amesema Mashirika hayo yanawajibu wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kifikra na maendeleo katika jamii kupita utekelezaji wa miradi yao mbalimbali.
“Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali, yamesajiliwa kisheria kwa lengo la kutoa huduma na elimu katika nyanja tofauti kwa jamii hivyo mtambue kwamba ajenda ya maendeleo endelevu katika Taifa ni pamoja na kuwa mawakala wa mabadiliko chanya katika jamii” amesema Dkt Jungu.