Featured Kitaifa

UCHUMI WA MAJIMBO UTAMKOMBOA MTANZANIA-MGOMBEA URAIS UMD

Written by Alex Sonna

MGOMBEA  urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Noty Mirambo,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 11,2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa jijini Dodoma, 

Na.Gideon Gregory-DODOMA


MGOMBEA  urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Noty Mirambo, amesema kuwa sera kuu ya chama chake ni kujenga uchumi wa majimbo ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika moja kwa moja na rasilimali, vitega uchumi, na miradi ya maendeleo inayopatikana katika eneo analoishi.

Akizungumza leo Agosti 11,2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo Njedengwa jijini Dodoma, Mirambo amesema  kuwa UMD inaamini katika mfumo shirikishi wa maendeleo unaompa mwananchi nguvu ya kiuchumi kutoka ngazi ya chini.

“Namshukuru Mungu kwa kukamilisha zoezi hili, ambalo ni hitaji la kikatiba- haki ya kupiga kura au kupigiwa kura. Sisi UMD sasa tuko tayari kuanza michakato ya uchaguzi, na kazi imeanza leo,” amesema Mirambo.

Hata hivyo ameeleza kuwa sera za UMD zinalenga kumwezesha kila mwananchi, kupitia uwekezaji wa moja kwa moja katika majimbo, pamoja na kuruhusu wananchi kushiriki katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za maendeleo.

“Tunataka majimbo yenye nguvu kiuchumi, ambapo wananchi wanamiliki maendeleo yao. Huu ndio mwelekeo wa UMD,” ameongeza

Mirambo aliwasili katika ofisi za INEC saa 5:00 asubuhi, akiwa ameambatana na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji pamoja na  viongozi wa chama na wapambe waliomsindikiza kwa shamrashamra za kidemokrasia.

About the author

Alex Sonna