Featured Kitaifa

MGOMBEA URAIS AAFP NA MWENZA WAKE WAKABIDHIWA FOMU

Written by Alex Sonna

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru,akipokea Begi lenye Fomu za kugombea nafasi ya Rais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele katika Ofisi za Tume hiyo Njedengwa Jijini Dodoma tarehe 09 Agosti, 2025. Kushoto ni Mgombea Mwenza Chumu Abdallah Juma.

Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, akionesha Begi lenye Fomu zake za kugombea nafasi hiyo mara baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele katika Ofisi za Tume hiyo Njedengwa Jijini Dodoma tarehe 09 Agosti, 2025.

Na.Alex Sonna-DODOMA

MGOMBEA wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwiru, pamoja na mgombea mwenza wake, Chumu Abdallah Juma, wamekabidhiwa fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi hiyo katika Makao Makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.

Ngombale alifika katika ofisi za INEC saa 9:53 alasiri akiwa ameambatana na mgombea mwenza pamoja na msafara wa magari madogo mawili na basi ndogo moja. Walipokelewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima, ambaye aliwaomba wasindikizaji wasiozidi 20 kuruhusiwa kuingia ndani kushuhudia zoezi hilo.
Baada ya kukamilisha zoezi la kupokea fomu, Ngombale aliwataka waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kumuombea katika safari ya kutafuta wadhamini katika mikoa kumi, ikiwemo minane ya Tanzania Bara na miwili kutoka Zanzibar (Unguja na Pemba), kama inavyotakiwa na taratibu za INEC.
Akielezea vipaumbele vya serikali yake iwapo atachaguliwa, Ngombale alisema:
“Serikali yangu itakuwa ya mchakamchaka yenye vipaumbele vitatu; cha kwanza ni uzalendo, pili uzalendo, na cha tatu ni uzalendo kwa taifa letu.”

About the author

Alex Sonna