Featured Kitaifa

THBUB YAHAMASISHA WANANCHI NA WADAU KWENDA KUPIGA KURA UCHAGUZI MKUU

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mohamed Khamis Hamad ametoa wito kwa wadau wa uchaguzi, Serikali na wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuwachagua viongozi.

Mhe. Hamad ameyasema hayo leo Agosti 7,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la tume hiyo lililopo katika Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni.

“Uchaguzi ni maendeleo kwasababu ni hatua moja ya kuwajibisha wale ambao hawajatekeleza majukumu yao vizuri, lakini kuwachagua viongozi watakao tuletea maendeleo katika taifa letu, “amesema.

Mbali na hilo amesema wao kama Tume wanaona hiyo ni hatua muhimu na wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuwachagua viongozi wanaoona wanafaa kwaajili ya maendeleo.

Pia, amewataka wadau wote wa uchaguzi kufuata sheria na taratibu zote za uchaguzi kwani haki ya kushiriki katika masuala ya uchaguzi haikujitengeneza yenyewe, ni haki inayotekelezwa kupitia miongozo ya sheria kutoka hatua ya mwanzo ya uandikishaji, elimu ya mpiga kura mpaka kampeni na siku yenyewe ya kupiga kura pamoja na kutangaza matokeo.

“Yote hayo yameelezwa kwenye sheria za nchi, kwenye Katiba sheria za uchaguzi na miongozo mingine, kwahiyo ni jukumu la wadau wote wa uchaguzi kufuata sheria za uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na vyombo ambavyo vimewekwa kusimamia uchaguzi, “amesema.

Aidha, Mhe. Hamad amesisitiza umuhimu wa kutunza amani ambayo inaweze watu kupata haki yao ya kushiriki kwenye uchaguzi na kupiga kura, kwani kukiwa na vurugu kutawanyima watu wengine haki hiyo ya kuchagua na kuchaguliwa.

About the author

mzalendo