Featured Kitaifa

SENYAMULE ATOA WITO KWA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUJITANGAZA ZAIDI

Written by mzalendo

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa wito kwa Wizara ya Katiba na Sheria kujitangaza zaidi ili wananchi waweze kujitojeza kwa wingi kupata Elimu na Msaada wa Kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayotekelezwa na wizara hiyo.

Senyamule ametoa wito huo Agosti 5, 2025 Jijini Dodoma wakati alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa maonesho ya wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nanenane Nzuguni.

Senyamule amesema kuwa wananchi wanatakiwa kunufaika na Msaada wa kisheria wakati huu wa maonesho kwa kuwa wamekuwa wakiwafuata watu ambao hawana uelewa na masuala ya Kisheria.

“Kama mko hapa mjitangaze ili wananchi waje kwa wingi, wapate huduma za Msaada wa Kisheria kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakitufuata lakini tunashindwa kuwasaidia kwa kuwa wengi wetu hatuna utaalam na masuala ya kisheria” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Msaada wa Kisheria, Osborn Paiss amefafanua kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inashiriki maonesho ya Nanenane kwa kuendelea kutekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia pamoja na kutoa elimu kuhusiana na Utajiri asilia na maliasili za nchi pamoja na elimu ya Haki za Binadamu na Utawala Bora bure.

“Tuko katika viwanja hivi vya Nanenane Nzuguni katika Maonesho ya Wakulima, tunaendelea kutoa huduma za Msaada wa Kisheria, Elimu kuhusiana na Utajiri Asilia na Maliasili za nchi, Haki za Binadam, Uraia na Utawala Bora, tunawakaribisha wanachi wote kuja kupata huduma maana zinatolewa bure kabisa” amesema Osborn.

About the author

mzalendo