Featured Kitaifa

MIGOGORO MBALIMBALI KUTATULIWA NA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KATIKA MAONESHO YA NANENANE

Written by mzalendo

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabiri Shekimweri amesema kuwa uwepo wa Wizara ya Katiba na Sheria katika maonesho na Sikukuu ya Wakulima kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma utawezesha kupunguza migogoro ya ardhi

Shekimweri ameyasema hayo leo Agosti 6, 2025 alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria na kuongeza kuwa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia utasaidia kupunguza migogoro hususan ya ardhi ambayo bado ni mingi katika mkoa wa Dodoma.

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwani wizara hiyo inashughulikia na kusikiliza kero, malalamiko na changamoto mbalimbali hivyo basi watumie fursa hiyo kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kutoka kwa wataalamu wa kisheria.

“Nimefurahi sana kukuta banda la Wizara ya Katiba na Sheria linatoa huduma hii ya Msaada wa kisheria lakini pia inatoa elimu hivyo natoa wito kwa wananchi wote wafike hapa kupata elimu na huduma ya utatuzi wa migogoro, lakini pia kinamama mjitokeze kwa wingi kujifunza Masuala ya mirathi kwani nyie ndio wahanga wa masuala hayo”, amesema.

Aidha Shekimweri amepongeza utiaji wa Elimu ya Haki na Utawala Bora inayotolewa kwani itawafaa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi Mkuu.

“Tunaelekea katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu kwahiyo wananchi wanaofika katika banda hili wananufaika na elimu hii itakayowasaidia kutambua wajibu na haki zao ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo,” amesisitiza Shekimweri.

About the author

mzalendo