DODOMA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za petroli zitakazotumika hapa nchini kuanzia Jumatano Agosti 6, 2025, zikionesha kupungua kwa bei ya petroli kwa shilingi 34 kwa mafuta yaliyopokelewa bandari ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara mtawalia.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile, imeeleza kuwa bei ya petroli katika soko la dunia imepungua kwa 2.3 % huku dizeli ikiongezeka 5.7 % na mafuta ya taa kwa 3.7%. Vilevile, taarifa hiyo imebainisha kuwa viwango vya kubadilisha fedha,kwa bei za mwezi Agosti, 2025, wastani wa gharama za kubadilidha za kigeni umepungua kwa asilimia 2.
Kwa upande wa gharama za kuagiza mafuta, kwa Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa 12.3% kwa petroli, 3.11% kwa dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa 13.08 % huku bandari ya Tanga kukiwa hakuna mabadiliko. Kwa bandari ya Mtwara, gharama zimeongezeka kwa 6.12% kwa mafuta ya petroli na 60.82% kwa dizeli.
Aidha, EWURA imewakumbusha wafanyabiashara kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.