WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, akizungumza wakati akifungua kongamano la siku mbili la kutathmini utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa katika ngazi ya mikoa na halmashauri iliyoanza leo Agosti 5,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, ametoa agizo kwa waratibu wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa katika ngazi ya mikoa na halmashauri kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu utekelezaji wa programu hiyo katika maeneo yao.
Dk. Gwajima ametoa agizo hilo leo Agosti 5,2025 wakati akifungua kongamano la siku mbili la kutathmini utekelezaji wa Programu hiyo, Dk. Gwajima,amesisitiza kuwa taarifa hizo ni muhimu kwa ajili ya ufuatiliaji, tathmini na kupanga mikakati ya maendeleo yenye tija.
“Taarifa zinazowasilishwa ni chombo muhimu cha kusaidia Serikali na wadau wake kujua wapi tumefika, changamoto zilizopo na nini kifanyike. Ni lazima waratibu wetu wawe na uelewa na uzingativu wa kutosha katika eneo hili,” amesema Dk. Gwajima.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali na wadau mbalimbali kama mashirika ya kiraia, taasisi binafsi na mashirika ya kimataifa katika kutekeleza programu hiyo, ili kufanikisha malengo ya kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi.
Hata hivyo Dk.Gwajima amewataka waratibu hao kuweka msukumo mkubwa katika kuimarisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa kuyaunganisha moja kwa moja na fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.
Dk. Gwajima amesema kuwa majukwaa hayo yameanzishwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kwa lengo la kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Majukwaa haya si ya kupuuzwa, ni fursa halisi kwa wanawake wa makundi yote. Nataka kuona waratibu wanayasimamia kwa nguvu, wanayahuisha na kuhakikisha wanawake wanapata taarifa, mafunzo na kuunganishwa na fursa za mikopo, masoko na teknolojia,” alisema.
Pia amesisitiza kuwa Programu ya Kizazi Chenye Usawa inalenga kubadili maisha ya wanawake na wasichana kupitia ujenzi wa mazingira wezeshi ya kiuchumi, kijamii na kisera. Hivyo, majukwaa hayo yanapaswa kuwa chombo kikuu cha utekelezaji wa lengo hilo.
Naye, akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Ofisa Programu Msaidizi wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa, Jackline Chomi amesema kuwa Tanzania imeonesha uongozi wa mfano katika kutafsiri malengo ya jukwaa hilo katika sera na programu za kitaifa.
“Tunaendelea kuona mafanikio makubwa, ikiwemo ongezeko la ushiriki wa wanawake katika sekta za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, pamoja na mafanikio katika kutumia teknolojia salama kwenye shughuli za kila siku,” amesema Chomi.
Amesema kuwa UN Women itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha mpango huo unaendelea kuleta mabadiliko chanya ya kudumu kwa wanawake na jamii kwa ujumla.