Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Athuman Kilundunya amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala katika ulinzi wa haki za binadamu haswa haki ya kuishi katika jamii zenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mhandisi Kilundunya ameyasema hayo Agosti 4,2025 wakati alipotembelea banda la THBUB katika Maonesho ya Nanenane Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Mhandisi Kilundunya ameeleza kuwa kati ya mambo ambayo Wizara ya Kilimo inapambana nayo ni migogoro iliyopo katika baadhi ya maeneo ya Wafugaji na Wakulima ambapo kuna wakati hupelelekea kuvunjwa kwa haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi.
“Tushirikiane katika kutatua migogoro, THBUB mnaweza kutuletea ushauri kutokana na chunguzi mnazozifanya zinazohusu masuala ya wakulima na wafugaji tusaidie ndugu zetu ” Alisema.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Elimu kwa Umma na Mawasiliano Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi.Zawadi Msalla amesema Wizara ya Kilimo ni kati ya wadau muhimu wa THBUB.
“Tumekuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara ya Kilimo na tunaahidi kuendelea kushirikiana katika usimamizi wa haki za binadamu” Alisema
Aidha, Bi. Zawadi alieleza kuwa THBUB imeshiriki katika maonesho ya Nanenane ili kutoa elimu,ushauri wa kisheria pamoja na kupokea malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora.