Na Mwandishi Maalumu – Lusaka,
Zambia
02/08/2025 Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Hakainde Hichilema ameipongeza Tanzania kwa kushiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia ambayo yametumika kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa kiafya na usafirishaji baina ya nchi hizo mbili.
Pongezi hizo amezitoa leo jijini Lusaka alipotembelea banda la Tanzania kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya ubingwa bobezi zinazopatikana nchini Tanzania pamoja na huduma za usafirishaji.
“Mhe Balozi amenipa maelezo mazuri kuhusu huduma za kibobezi zinazotolewa na Taasisi ya MOI, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, hakika huduma zinazotolewa ni za kiwango cha kimataifa, hongereni sana”, alisema Mhe. Rais Hichilema.
Mhe. Rais Hichilema amesema kushiriki kwa Tanzania katika maonesho hayo ni ishara kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili ni mkubwa na unalenga kuwasaidia wananchi.
“Nafurahi kuwaona Tanzania Ports Authority na Air Tanzania, tunawashukuru kwa huduma zenu za uchukuzi na usafirishaji, Zambia tunatambua mchango wenu katika uchumi wetu una ustawi wa Wananchi wetu” – Mhe. Rais Hichilema.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule amemshukuru Mhe. Rais Hichilema kwa kutembelea banda hilo na kusema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika maonesho hayo kwa kuonesha huduma mbalimbali zinazopatikana nchini humo.
Aidha, Balozi Mkingule amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Zambia bila vikwazo, ikihakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa nchini Tanzania zinawafikia wananchi wa Zambia na wanufaike nazo kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Katika banda hili kuna taasisi kubwa tano ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Ndege la Air Tanzania ambazo zinatoa huduma za afya na usafirishaji”.
Tanzania imeshiriki katika maonesho hayo ikiwa na lengo la kutangaza huduma za matibabu ya kibingwa na huduma za usafirishaji zinazopatikana nchini kwa wananchi wa Zambia na mataifa mengine yanayoshiriki katika maonesho hayo.