Featured Kitaifa

INEC YAWAFUNDA WAZALISHAJI WA MAUDHUI MTANDAONI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele ametoa wito kwa wazalishaji wa maudhui mtandaoni kuhakikisha taarifa zinazopandishwa katika kurasa zao zinakuwa za kweli na zisizo na chembe ya upotishaji ili kupeuka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Jaji Mwambegele ametoa wito huo leo Agosti 3,2025 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi na wazalishaji maudhui mtandaoni kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Nawasisitiza na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya akili unde ambayo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia hovu kusambaza habari za upotoshaji hasa kupitia mitandao ya kijamii,”amesema.

Ameongeza kuwa tume hiyo ina matumaini makubwa na vyombo vya habari katika kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu kupitia ushiriki wao.

“Imani hii inatokana na ushirikiano wenu mliouonesha tangu awali kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga, mmekuwa wepesi wa kuwasilisha hoja na ushauri pale inapohitajika kila tunapokutana nanyi kwenye vikao,”ameongeza.

Akiwasilisha mada kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na ushiriki wa vyombo vya habari Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima amesema Tume inatarajia vyombo vya habari vitatumia kalamu zao na nyenzo walizonanzo kuhubiri amani katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

“Tunawaomba na kuwasihi, kutumia nafasi na fursa mlizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu uchaguzi, “amesema.

Pia ameongeza kuwa vyombo vya ndivyo vinaweza kuwa sauti ya kwanza ya kuonesha upotoshwaji wa aina yoyote unaofanywa kwa bahati mbaya au makusudi kuhusu Tume na zoezi la uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Tume imejiwekea utaratibu wa kuvishirikisha vyombo vya habari katika mchakato mzima wa uendeshaji wa uchaguzi huu ili kuweka uwazi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu, “ameongeza.

About the author

mzalendo