Featured Kitaifa

TARURA YASHIRIKI MAONESHO YA NANE NANE NZUGUNI JIJINI DODOMA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inashiriki Maonesho ya Nane Nane kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Nzuguni jijini Dodoma.

TARURA inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu kazi na majukumu yake pamoja na kupokea maoni na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TARURA Bi. Catherine Sungura amesema kuwa TARURA imejipanga kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali wanayoyasimamia yanayohusu ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini.

Kwa mujibu wa Bi. Sungura baadhi ya maeneo hayo ni pamoja usimamizi wa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya maeneo korofi shughuli za maabara,mazingira na jamii.

“Kupitia wataalamu wetu ambao wapo katika banda letu tumejipanga pia kutoa elimu kwa wananchi na wadau wetu wengine namna wanavyoweza kushirikiana na TARURA kuwezesha matengenezo madogo madogo ya barabara kupitia vikundi vya kijamii” amefafanua Bi. Sungura

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutembelea Banda la TARURA na mabanda mengine ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambayo yanapatikana katika hema linalosomeka “Government Zone Pavilion 2” ili wapate elimu na ufahamu kuhusu taasisi hizo.

About the author

mzalendo