Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wa Rais, Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara utakaofanyika Oktoba 29, Wizara ya Katiba na Sheria imesema kupitia maonesho ya Nanenane mwaka huu watatoa elimu ya katiba na sheria za uchaguzi huo.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kwa umma kutoka Wizara hiyo Mhe. Abdulrahman Msham wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya 32 ya kitaifa ya Wakulima, Wavuvi na Wafugaji Nanenane na ya 3 kimataifa mwaka 2025.
“Mbali na hilo tunayo kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambapo hapa tunashugulikia migogoro, tunatatua migogoro na tunatoa ushauri, vile vile hata ukiwa na maombi yako ya kuongezewa muda kwaajili ya kufungua mashauri unaruhusiwa kufika katika banda hili na huduma zote utazipata,”amesema.
Amesema Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na mambo mengine inasimamia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kwani wanatoa huduma za usajili kuwa mtatuzi wa migogoro kama njia mbadala pamoja na elimu kwa kutumia njia hiyo.
“Lakini vile vile utapata elimu ya haki za binadamu na ulinzi wa maliasili na utajiri asilia wa nchi, vitu vyote hivyo vinapatikana katika banda letu,”amesema.
Sambamba na hayo ametumia wasaha huo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda hilo ili wapate huduma kwani wanao wataalamu kwaajili ya kuwahudumia.
“Ukifika katika banda letu utahudumiwa na changamoto zako zote zitamalizika hapa hapa katika banda letu lililopo katika viwanja hivi vya Nanenane,”amesema.
Maonesho ya Nanenane ya mwaka 2025 yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.
Kaulimbiu hiyo imechaguliwa mahsusi ili kukumbusha umuhimu wa viongozi bora katika kuinua uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, 2025.