Featured Kitaifa

UKOSEFU WA MAADILI NGAZI YA FAMILI WATAJWA CHANZO CHA KUKITHIRI VITENDO VYA RUSHWA

Written by Alex Sonna

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila wakati akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na Utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya kitaaluma.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Felista Shuli akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na Utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya kitaaluma.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na Utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya kitaaluma. 

Na Gideon Gregory, Dodoma

Imeelezwa kuwa kukosekana kwa maadili katika ngazi ya familia ndiyo chanzo cha kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi Serikali na sehemu zingine.

Hayo yameelezwa leo Julai 30,2025 hapa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila wakati akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na Utawala bora baina ya taasisi simamizi za maadili ya kitaaluma.

“Ni rai yangu kuwa tulione na tulijadili tatizo la mmomonyoko wa maadili kwa mapana yake na tujiwekee mikakati ya pamoja itakayo tuwezesha kudhibiti uwepo wa vitendo vya rushwa katika utumishi wa umma,”amesema.

Aidha, amewaomba washiriki wa kikao hicho kuendelea kushirikiana na kuwekeza katika mikakati ambayo itaakisi na kuimarisha utendaji kazi wa wataalam wanaotoa huduma kwa wananchi.

“”Ili kwa pamoja tuweze kufikia hazma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuona tunakuwa na utumishi wa umma wenye usikivu na uwajibikaji wa hiali kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania, hivyo natoa rai kwamba mawasilisho na majadiliano yetu yatuongoze kwenye ubunifu na mikakati kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma kama njia moja wapo ya kuimarisha utoaji wa huduma katika utumishi wa umma, kudhibiti vitendo vya rushwa kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi, “amesema.

Amesema pamoja na utekelezaji wa malengo hayo mahususi, amewasihi kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati ya taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma ili kuimarisha hali ya uadilifu katika taasisi na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaonekana kwenda kinyume na taratibu zilizotolewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamizi wa maadili, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Felista Shuli amesema kwa mujibu wa tafiti walizofanya mwaka 2022 hali ya maadili imezidi kuimarika nchini licha ya cha kuendelea kuwepo kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha.

“Bado changamoto zipo kutokana na mitindo ya maisha ambayo tunayo kwasababu maadili yanaanza na familia, yanakuja kwenye ngazi ya shule na yanakuja mpaka kazini na sisi utumishi wa umma tunasimami tayari yule mtumishi ambaye amekwisha toka kwenye familia,”amesema.

Pia Bi. Shuli ameongeza kuwa suala hilo ni mtambuka ambapo pamoja na utafiti huo uliofanyika mwaka 2022 wanategemea kufanya utafiti mwingine ili waweze kuona baada ya muda huo kama kuna mabadiliko.

About the author

Alex Sonna