Featured Kitaifa

‎CCM YATANGAZA MAJINA YA WALIOPITISHWA KWA UTEUZI WA AWALI,MPINA NA MAKAMBA WATUPWA NJE

Written by Alex Sonna

 

‎Na Meleka Kulwa – Dodoma

‎Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza uteuzi wa awali wa wagombea wa nafasi za ubunge kwa majimbo yote 272 ya Tanzania Bara na Visiwani. Katika mchakato huo, jumla ya wagombea zaidi ya 5,000 wamejitokeza kuwania ubunge huku zaidi ya 30,000 wakichukua fomu kuwania nafasi za udiwani.

‎Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 29, 2025 jijini Dodoma na CPA Amos Makalla, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi za Chama hicho ( White House) , CPA Amos Makalla amesema uteuzi huo umefanywa kwa kuzingatia sifa, uwezo wa mgombea, na mahitaji ya kisiasa ya majimbo husika.

‎Chama pia kimetoa wito kwa wale ambao hawakupata nafasi kwa sasa kutokata tamaa, bali waendelee kukiunga mkono CCM kwani nafasi za kulitumikia chama bado ni nyingi.

‎CPA Amos Makalla ametangaza rasmi majina ya wagombea watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 kwa nafasi za Ubunge wa Majimbo, Viti Maalum na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

‎Amesema uteuzi huo, uliofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, umehusisha majimbo 272 upande wa Tanzania Bara na umehitaji umakini mkubwa kutokana na wingi wa maombi ya wagombea.

‎Majimbo zaidi ya elfu tano yalipokea maombi ya wagombea. Kazi hii ilikuwa kubwa na ilihitaji umakini mkubwa. Kwa wale ambao hawajapata uteuzi, tunawaomba waendelee kuwa watiifu kwa chama kwani bado CCM inawathamini,” amesema CPA Makalla.

‎Baadhi ya majimbo yanatazamiwa kuwa na ushindani mkali kutoka kwa wagombea. Majimbo hayo ni pamoja na Jimbo la Mtama walikopita Nape Nnauye, Jemedari Said na wengineo; Jimbo la Kigoma Mjini ambapo wanahabari Baruan Mhuza na Baba Levo wametajwa; huku Salim Kikeke akipitishwa kugombea Jimbo la Moshi Vijijini.

‎Aidha, baadhi ya vigogo akiwemo Luhaga Mpina, January Makamba, Askofu Josephat Gwajima na Mrisho Gambo hawajarejea kwenye orodha ya mwisho ya wagombea, hatua inayotafsiriwa kama mabadiliko makubwa ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.

‎CPA Makalla amesisitiza kuwa vigezo vya uadilifu, uwezo wa uongozi na kukubalika kwa wananchi vilizingatiwa ili kuhakikisha chama kinapata wagombea bora watakaotekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM na kuendeleza kasi ya maendeleo ya Taifa.

‎Kwa upande mwingine CPA Amos Makalla amesema Chama Cha Mapinduzi kipo tayari kwa uchaguzi Mkuu.

About the author

Alex Sonna