Na Alex Sonna, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omary,amefungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa magereza na wataalam wa elimu ya watu wazima kuhusu uhamasishaji wa kampeni ya madarasa ya kisomo nchini.
Mafunzo hayo yameanza leo Julai 28 ,2025 jijini Dodoma yakilenga kupunguza idadi ya watu wasio na stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kutumia mbinu za kisasa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Omary amesema Tanzania bado ina asilimia 17 ya watu wasio na stadi za KKK, hali inayokwamisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza changamoto hiyo, ikiwemo kuimarisha elimu nje ya mfumo rasmi kupitia programu kama MUKEJA, IPOSA na elimu ya sekondari mbadala.
“Tunataka wananchi wetu wapate ujuzi wa kusoma na kuandika huku wakipata stadi za amali zitakazowawezesha kushindana kwenye soko la ajira na kujitegemea kiuchumi,” amesema Dkt.Omary, akisisitiza matumizi ya mbinu ya RIFLEKTI inayowasaidia walengwa kubaini changamoto na kupata ufumbuzi huku wakijifunza KKK.
Aidha, ametoa wito kwa wataalamu wa elimu ya watu wazima kuhakikisha programu za kisomo zinasimamiwa kwa ufanisi ili kupunguza ujinga, umaskini na maradhi kama alivyoasisi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia kampeni mbalimbali za kitaifa.
Amepongeza pia jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ikiwemo fedha za ujenzi wa vituo na karakana za mafunzo ya amali kwa vijana na watu wazima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo na yanalenga kuwapa wawezeshaji mbinu mpya za ufundishaji.
“Kwa kutumia mbinu ya RIFLEKTI, tunawapa walengwa ujuzi wa maisha, stadi za ujasiriamali na maarifa ya kisasa ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na Taifa,” amesema Prof. Sanga.
Prof. Sanga ameongeza kuwa Serikali kupitia TEWW imefanikisha kurejesha wasichana takribani 13,000 waliokatisha masomo na vijana zaidi ya 42,000 wamepata elimu kupitia programu ya IPOSA katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mafunzo hayo yameshirikisha viongozi wa elimu wa mikoa na wilaya, maafisa magereza kutoka mikoa mbalimbali, pamoja na wataalamu wa elimu ya watu wazima, yakiwa na lengo la kuimarisha kampeni ya madarasa ya kisomo na kupunguza ujinga nchini kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.