Featured Kitaifa

ELIMU BILA MIPAKA:TEWW YATIMIA MIAKA 50 YA KUINUA

Written by Alex Sonna

WAZIRI wa  Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 26,2025 jijini Dodoma kuhusu  ya  maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW),yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam.

WAZIRI wa  Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 26,2025 jijini Dodoma kuhusu  ya  maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW),yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam.

Na Alex Sonna, Dodoma
Wakati Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ikiadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, jamii ya Watanzania imeendelea kushuhudia mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi yanayotokana na elimu nje ya mfumo rasmi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, elimu ya watu wazima imekuwa chachu ya maendeleo kwa maelfu ya wananchi waliopata nafasi ya pili ya kujifunza, kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi kupitia maarifa ya kisomo, ufundi na ujasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Prof. Mkenda alieleza kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW, yaliyozinduliwa rasmi wiki hii, yanabeba kauli mbiu isemayo “Elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu” ikiwa ni wito kwa jamii kutambua kuwa hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma kwenye safari ya maarifa.
“Elimu ya watu wazima ni nguzo muhimu kwa wale waliokosa fursa katika mfumo rasmi. TEWW imekuwa daraja la matumaini kwa watu waliodhani wamechelewa—lakini sasa wanaandika, wanajua hesabu, wanauza bidhaa zao kwa ufanisi, na wanachangia uchumi wa nchi,” alisema Waziri.
Katika kuendeleza mafanikio hayo, Serikali kupitia TEWW imeandaa mafunzo maalum kwa Maafisa Magereza na Wakufunzi wa Taasisi hiyo, yatakayofanyika Julai 28–30, lengo likiwa ni kuimarisha programu za kisomo kwa wafungwa na watu walioko pembezoni mwa mfumo rasmi wa elimu.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Agosti 25–27, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Kongamano hilo la siku tatu litawakutanisha zaidi ya wadau 1,000 wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika maonesho yatakayofanyika JNICC kuanzia Agosti 24, wananchi watajifunza kuhusu huduma mbalimbali za elimu ya watu wazima, kushuhudia ubunifu wa vijana waliopitia mafunzo ya TEWW, pamoja na kupata fursa za udahili na ushauri wa kitaaluma.
Wanawake na vijana waliopitia mfumo huo wamekuwa wakionesha mafanikio makubwa katika biashara ndogondogo, useremala, ushonaji, utengenezaji wa bidhaa asilia, teknolojia rahisi na huduma nyingine za kijamii, hali inayoendelea kubadilisha maisha yao.
“Elimu isiyo rasmi imetufungua macho. Niliwahi kufukuzwa shule nikiwa mdogo, lakini kupitia TEWW sasa najua kusoma, kuandika na nimeshafungua duka langu mwenyewe,” alisema Rose Mligo, mshiriki wa mafunzo ya elimu ya watu wazima kutoka Mkuranga.
Waziri Prof. Mkenda alihitimisha kwa kuhamasisha jamii yote kushiriki katika shughuli za maadhimisho hayo, akisisitiza kuwa “kila Mtanzania ana haki ya kupata maarifa, bila kujali umri, jinsia au nafasi alipo katika jamii.”

About the author

Alex Sonna