Featured Kitaifa

WAJUMBE WA KAMATI JUMUISHI YA UENDESHAJI PROGRAMU YA MIFUMO HIMILIVU YA CHAKULA ‘TFSRP’ WAKUTANA PEMBA

Written by mzalendoeditor
Wajumbe wa Kamati Jumuishi ya Uendeshaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) wamekutana katika Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa programu hiyo inayolenga kuimarisha usalama wa chakula kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Bwana Ali Khamisi Juma, alisema chanzo kikuu cha programu hiyo ni hitaji la kutumia rasilimali ardhi, maji, na mazingira kwa njia endelevu ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mradi huu unatufundisha namna ya kutumia teknolojia sahihi zitakazotuwezesha kuzalisha kwa tija kubwa kwenye eneo dogo bila kuharibu ardhi,” amesema Juma.
Kwa upande wa Zanzibar, amesema kuwa programu imejikita zaidi kwenye ukarabati wa miundombinu ya kilimo na maandalizi ya hekta 8,000 za ardhi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa chakula, sambamba na maeneo ya kiutendaji na uendeshaji wa programu hiyo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amewahimiza wananchi kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa TFSRP na kuzitaka sekta binafsi kushiriki kikamilifu, hasa kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji.
“Ushiriki wa sekta binafsi ni hatua muhimu ya kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 ambayo inaipa nafasi kubwa sekta hiyo katika maendeleo ya kilimo,” amesisitiza.
Kwa upande wa Tanzania Bara, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Ndugu Obadia Nyagiro, amesema utekelezaji wa programu hiyo ulianza rasmi mwaka 2023 kwa gharama ya jumla ya Dola za Marekani milioni 300, ambapo Zanzibar inatekeleza kwa bajeti ya milioni 15 na Bara milioni 285.
Amesema programu imejikita katika kuongeza uzalishaji wa chakula ili kukabiliana na changamoto ya ongezeko la watu huku ardhi ikiwa haiongezeki. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, idadi ya watu inakadiriwa kufikia kati ya milioni 79 hadi 80 mwaka 2030, na kufikia milioni 136 mwaka 2050.
“Tunahitaji teknolojia bora za kilimo katika hatua zote za uzalishaji ili kuhakikisha chakula cha kutosha kinapatikana kwa wote. Hii ni pamoja na ukarabati wa miundombinu, utafiti wa mbegu, huduma bora za ugani na kulinda afya ya udongo,” amesema Nyagiro.
Aidha, utekelezaji wa TFSRP unaenda sambamba na Azimio la Kampala (CADP) la mwaka 2025, ambalo linapigia chapuo mkakati wa Afrika wa kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030.
“Lengo kuu ni kuhakikisha nchi za Afrika zinazalisha chakula cha kutosha na kuwa na ziada ya kuuza kwa mataifa jirani,” amesema.

About the author

mzalendoeditor