Na Mwandishi Wetu, Singida
Uchimbaji na uchakataji wa madini ya gypsum katika Wilaya ya Itigi, mkoani Singida, umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo, hususan vijana na wanawake, huku Serikali ikihamasisha wawekezaji kuja kuwekeza zaidi katika sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini, Mkaguzi wa Madini Ujenzi na Viwandani Itigi, kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Charles Fumbuka, amesema shughuli za uchimbaji wa gypsum zinafanyika kwa usalama na kuwanufaisha wananchi kwa kuongeza ajira na kipato.
“ Wachimbaji wameitikia wito wa Serikali wa kuongeza thamani madini yao hapo hapo mgodini badala ya kusafirisha madini ghafi. Gypsum sasa inatengeneza mikanda ya gypsum kwa ajili ya ujenzi wa nyumba pamoja na bidhaa mbalimbali ambazo huuzwa ndani na nje ya Nchi,” amesema Fumbuka.
Aidha, amesema masoko ya bidhaa zinazotokana na gypsum yanapatikana ndani ya mkoa na yanaendelea kuimarika kadri mahitaji ya viwandani yanavyoongezeka.
Kwa upande wake, Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Mutagwa, amesema mkoa wa Singida una utajiri mkubwa wa madini na fursa lukuki kwa wawekezaji, hasa kwenye viwanda vya saruji na bidhaa za ujenzi.
“Singida ni mkoa wenye rasilimali nyingi. Tuna gypsum ya kutosha, nguvu kazi ya kutosha, na wananchi wenye ushirikiano mkubwa. Tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza, hasa kwenye viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani ya madini yetu,” amesema Mutagwa.
Naye mchimbaji wa madini ya gypsum, Sadiki Kidira, amesema kuwa iwapo mazingira ya uchimbaji na uchakataji yataendelea kuboreshwa, Tanzania haitaendelea kuagiza gypsum kutoka nje ya nchi.
“Itigi tunaweza kabisa kuzalisha madini ya gypsum ya kutosha kwa matumizi ya ndani na hata kuuza nje. Vijana watanufaika zaidi na itapunguza changamoto za ajira na hata uvunjifu wa amani,” amesisitiza Kidira.
Mchimbaji mwingine mdogo, Moza Hilari, ameeleza namna alivyonufaika na uchimbaji huo, akisema ameweza kumsomesha mtoto wake na kujikimu kimaisha.
“Ninaishukuru Serikali kwa kutuamini na kutupa nafasi ya kushiriki kwenye Sekta ya Madini. Sasa tunaweza kujitegemea na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa taifa,” amesema Moza.
Kwa ujumla, uchimbaji na uchakataji wa madini ya gypsum Itigi si tu umeleta ajira, bali pia umefungua milango ya maendeleo endelevu kwa wananchi wa Singida – na sasa ni fursa kwa wawekezaji kuchangamkia madini haya yenye thamani.