Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Maswi amesema kuwa Haki si Hisani bali ni msingi wa Amani, Maendeleo na Mshikamano wa Kitaifa. Ameyasema hayo leo Julai 23,2025 wakati akifungua rasmi Kongamano la Msaada wa Kisheria la mwaka 2025 linalofanyika kwa siku mbili (23-24 Julai) katika Ukumbi wa Lush Garden Jijini Arusha.
Ndg. Maswi amesema kuwa ni jukumu la serikali na wadau kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinawafikia wananchi walengwa hususani walio pembezoni ili kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wanyonge unaimarishwa ili kujenga jamii inayotambua haki, usawa, kulinda na kuhifadhi amani na hatimaye kuongeza uelewa wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
‘’Tanzania ni nchi inayopambana katika masuala ya upatikanaji wa haki, ndio maana Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassa alikuwa huru kutumia jina lake katika utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wote’’ alisema Maswi.
‘’Dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi hususani wasio na uwezo wa kifedha na wale walio pembezoni wanafikiwa na kupata haki kwa wakati na kwa usawa mbele ya sheria na hiyo ndio maana halisi ya 4Rs” aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi alisema kuwa haki haitakiwi kusubiriwa bali inatakiwa ipelekwe kwa wananchi kwa wakati, kwa lugha inayoeleweka na kwa njia inayoweza kuwafikia wananchi wa hali zote.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi. Hanifa Said alisema kuwa Kongamano la Msaada wa Kisheria la Mwaka 2025 ni jukwaa mahususi la kuimarisha juhudi za utoaji huduma ya msaada wa kisheria kwa watanzania wote hususani makundi yaliyo katika mazingira magumu.
Akitoa salam kutoka Chama cha wanasheria Tanganyia-TLS, Rais wa TLS Wakili Boniphace Mwabukusi alisema kuwa huduma ya msaada wa kisheria haipaswi kuwa jambo la hiari bali wajibu wa kitaifa ambapo alitoa wito kwa wanasheria kusimama upande wa wananchi wanyonge na kuwa Daraja la wao kuifikia haki.