Na Mwandishi Wetu, Singida
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa daraja la Masagi linalojengwa katika barabara ya Kibirigi-Masagi kutasaidia kuunganisha vijiji vya Kibirigi, Masagi na Tyeme katika Kata ya Mtoa, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahim Kibasa wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo mbele ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA inayofanya ziara ya Ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa Miundombinu ya barabara mkoani humo.
“Vijiji vya Kibirigi, Masagi na Tyeme vinajishughulisha na shughuli za kilimo hususani pamba, alizeti, dengu, mahindi pamoja na ufugaji, hivyo kukosekana kwa daraja katika Mto sekenke linapojengwa daraja hilo ilikuwa ni kikwazo kwao katika kuyafikia masoko ya mazao yao na kurudisha nyuma jitihada za kujiletea maendeleo”. amefafanua Mhandisi Kibasa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kibasa kukamilika kwa Mradi huo utachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika vijiji hivyo na kuchangia ustawi wa maendeleo ya Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Mhandisi Kibasa ameileza Kamati hiyo kuwa licha ya changamoto ya mvua iliyojitokeza katika hatua ya utekelezaji, mradi huo umefikia hatua ya kuridhisha na matarajio yake ni kuwa utakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA Ally Rashid amemtaka Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida na timu yake kuendelea kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo kuzingatia ubora sambamba na kuyafanyia kazi mapungufu kadhaa waliyoyabaini wakati wa Ukaguzi wao katika Mradi huo.