Featured Kitaifa

WAZIRI AWESO ATAKA WAKANDARASI WAZAWA KUONESHA THAMANI YA FEDHA KATIKA UTEKELEZAJI MIRADI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka wakandarasi wa mradi wa maji wa miji 28 katika miji ya Wanging’ombe na Makambako mkoani Njombe kuonesha thamani ya fedha kwa kutekeleza mradi kwa wakati, weledi, ubora na viwango vinavyostahili. 

Amesema hayo baada ya kukagua miradi hiyo na kutoridhishwa na na kasi ya utekelezaji ya wakandarasi hao. 

Waziri Aweso ambaye ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema serikali ya awamu ya Sita inaimani kubwa na wakandarasi wazawa katika “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” hivyo imekuwa ikitoa kipaumbeke kwao katika kutekeleza miradi ya maji. 

Amesisitiza kuwa serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha fedha na stahili zote zinatolewa kwa wakati ili mradi ukamilike kwa wakati lakini bado kasi ya utekelezaji haifiki katika matamanio ya wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Wanging’ombe Mhandisi Fabian Maganga amesema mradi huo umefika asilimia 47.3 tofauti na matarajio ya awali ambapo mradi ulipaswa kuwa zaidi ya asilimia 80.

Waziri Aweso amemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka kufuatilia na kuchukua hatua zikiwemo hatua za kinidhamu kwa yeyote anayekwamisha kukamilika kwa mradi na kutoa sharti kwa wakandarasi kufanya kazi kwa saa 24 ili kufidia mapungufu yaliyojitokeza. 

Mradi wa maji wa Wanging’ombe unatekelezwa na Kampuni ya Larsen& Taubro LTD ambayo imetoa kandarasi kwa kampuni za Tanzania katika maeneo tofauti tofauti ya mradi.  

About the author

mzalendoeditor