Featured Kitaifa

WAKAZI 1,400 WA KIJIJI CHA NANGANO WAANZA KUPATA MAJI SAFI NA SALAMA

Written by mzalendoeditor

Tenki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa mita za ujazo 50,000 katika mnara wenye urefu wa mita3 linalohudumia wananchi wa kijiji cha Nangano Wilayani Liwale.

Na Mwandishi Wetu,Liwale

ZAIDI ya wakazi 1,428 wa kijiji cha Nangano Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi,wameanza kunufaika na matunda ya Serikali ya awamu ya sita baada ya kujengewa mradi wa maji ya bomba uliomaliza mateso ya wananchi hao kutembea umbali zaidi ya kilometa 3 kwenda kuchota maji katika Mto Mbwemkuru.
Mradi huo umejengwa na kampuni ya Epic Contruction Ltd, na kusimamiwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA)Wilaya ya Liwale kwa gharama ya Sh.milioni 461,448,578.55 zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya maji huku wananchi wa kijiji hicho wamechangia Sh.6,000,000.
Kwa mujibu wa meneja wa Ruwasa Wilayani Liwale Mhandisi Luhumbika Bunyataka ni kwamba,utekelezaji wa mradi wa maji Nangano umehusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa mita za ujazo 50,000 katika mnara wenye urefu wa mita3 na ujenzi wa vituo 5 vya kuchotea maji.
Ruhumbika alitaja kazi zingine zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii(CBWSO),ununuzi na ulazaji wa bomba kuu za kusambaza maji,kufunga pampu ya kusukuma maji,kufunga umeme jua na ujenzi wa nyumba ya mitambo na uzio.
Alisema,lengo la kujenga wa mradi huo ni kusogeza huduma ya majisafi na salama karibu na wananchi wa kijiji hicho katika umbali usiozidi mita 400 na kuboresha afya za wananchi ambao awali walilazimika kutumia maji ya visima vya asili na mito ambayo maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Aidha alisema,katika mradi huo kuna Jumuiya ya watumia maji ngazi ya jamii ambao wamekubaliana wenyewe kuchangia Sh.30 kwa ndoo moja ya lita 20 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa mradi husika na fedha zinazokusanywa zinapelekwa benki ya Jumuiya ili kuwa na usimamizi bora wa fedha hizo.
Mkazi wa kijiji cha Nangano Rehema Mkwepu,ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umemaliza mateso ya muda mrefu kutumia maji ya mito na visima pamoja na wanyama wa porini wakiwemo nguruwe na tembo.
“Tangu Uhuru wa Tanganyika na sasa Tanzania mwaka 1961 hatukuwahi kupata mradi wa maji ya bomba katika kijiji chetu, badala yake maji ya bomba tulitumia pindi tunapokwenda makao makuu ya Wilaya Liwale mjini au Hospitali ya Wilaya hivyo mradi huo umeleta faraja kubwa kwetu”alisema.

About the author

mzalendoeditor