Featured Kitaifa

FAMILIA ILIYOGOMA KUZIKA NDUGU YAO YAKUBALI YAISHE

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma

Familia iliyokuwa imegoma kuzika mwili wa Marehemu aliyefariki kwa Kupigwa risasi na askari Polisi, wamefikia makubaliano na Jeshi hilo  na kuendelea na taratibu za mazishi huku wakisisitiza kuwa wana imani na Jeshi hilo na haki itapatikana. 

Familia hiyo ni ya kijana Frank Sanga mwenye umri wa miaka 33 ambapo ndugu wligoma kuzika mwanzoni kutokana na utata baina ya familia na Jeshi la Polisi, ambapo kwa sasa wamekubali kuzika  na kuongeza kuwa kuendelea kugoma kuzika ni sawa na  kuendelea kumtesa Marehemu  kitu ambacho kwao siyo uungwana.

Mazishi hayo yamefanyika leo July 23,2025 nyumbani kwao Busena Kata ya Matumbulu Jijini Dodoma.

Kaka wa marehemu Alen Sanga amesema mwanzoni waligoma kuzika kwasababu walitaka kujua hatma ya ndugu yao, hivyo wamekubali kuzika wakiamini jeshi la polisi litaungana nao ili kuhakikisha wanapata haki ya marehemu.

“Tunaamini jeshi la polisi watalifuatilia suala hili, kisha ndugu yetu atapata haki zake,”anasema.

Aidha ameongeza kuwa baada ya wao kukaa na Jeshi la Polisi hawana suala la kuongea ila wanalipeleka mahakamani ndipo kwenye haki na kuongeza kuwa watafanya jitihada za kutafuta Mwanasheria kisha wataenda kusimama mahakamani.

‎Akiongoza ibada ya mazishi hayo Mchungaji wa Kanisa la Anglikan Nason Mjimbu ameitaka jamii kuhakikisha nchi inabaki kuwa salama na amani.

“Jambo hili lililotukusanya hapa la Frank kwetu sisi litukumbushe kuitafuta amani, tuishi kwa amani, Tanzania pawe mahali pa makimbilio kwa mataifa yote,”amesema.

Pia ameomba kuwa katika tukio hilo wasemaji wawe wachache na wasiwe wengi, na kuongeza kuwa wale waliopewa nafasi na dhamana ya kulinda wananchi na mali zao kila mtu asimame kwa nafasi yake.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mwenyekiti wa Mtaa Busena Alfred Lumorwa amewahasa vijana kuwa watulivu na kufuata utaratibu pindi yanapotokea matukio yenye kuleta taharuki.

Huku baadhi ya waombolezaji wakiiangukia Serikali iweze kuisaidia familia ya marehemu kwani kijana huyo alikuwa tegemeo.

Marehemu Frank Sanga alifariki July 19 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya DCMC Jijini Dodoma baada  ya kupigwa risasi na askari Polisi Ambao kwa sasa wanashikiliwa na Jeshi hilo kwa taratibu za kisheria huku akiwa ameacha Mjane na Watoto Wanne.

About the author

mzalendo