Featured Kitaifa

BENKI YA DUNIA KUJENGA MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME WA KV 400 KUTOKA UGANDA HADI TANZANIA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba (wa pili kushoto), Mtaalam wa Nishati kutoka Ofisi ya Benki ya Dunia nchini Tanzania Dkt. Rhonda Jordan (wa pili kutoka kulia), Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kulia) na Mhandisi Mkuu wa Nishati, John Magheni wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufanya mazungumzo katika Ofisi za Wizara ya Nishati Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Julai 23, 2025.

….

Benki ya Dunia (WB) imeeleza kuwa itatoa fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha  umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 400 kutoka nchini Uganda hadi Tanzania.

 Hayo, yameelezwa na Mtaalam wa Nishati kutoka Ofisi ya Benki ya Dunia nchini Tanzania, Dkt. Rhonda Jordan wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba katika Ofisi za Wizara ya Nishati Mji wa Serikali Mtumba Julai, 23 Jijini Dodoma.

 Dkt. Rhonda amesema kuwa kwa sasa benki hiyo imeridhia kutekeleza mradi huo baada ya kujiridhisha kuwa hauna athari za kimazingira kama ilivyokuwa ikielezwa hapo awali.

“Bodi ya Wakurugenzi sasa itapitisha fedha kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo, ambao ulikuwa ukisuasua kutekelezwa kwa madai ya kuathiri mazingira, lakini sasa bodi imeridhika na itatoa fedha za
kuanza kuutekeleza”, amesema Dkt. Rhonda

Katika hatua nyingine, Dkt. Rhonda ameialika Wizara ya Nishati kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Jijini New York nchini Marekani mwezi Semptemba, 2025.

Katika mazungumzo yao, Katibu Mkuu Mramba amemueleza Dkt.Rhonda kuwa wataendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika miradi mbalimbali ya Nishati ikiwemo ule wa usafirishaji umeme wa Tanzania-Zambia (TAZA) na mingine inayofafana kama hiyo.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na  Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga na Mhandisi Nishati Mkuu John Mageni.

About the author

mzalendoeditor