Na Prosper Makene, Arusha
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Hamis Mwinjuma ameipongeza Kampuni ya CRCEG ya kutoka nchini China ambayo inajenga uwanja wa mpira wa miguu jijini Arusha utakaotumika kwa michuano ya AFCON 2027 kwa kuweza kujenga uwanja huo kwa kasi na viwango vya hali ya juu.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa halfa ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa zege na kuanza rasimi kufunga paa la uwanja huo, Naibu Waziri amesema kuwa ni mara ya kwanza nchini kuona mkandarasi anamaliza kazi aliyopewa kabla ya muda kwani amemaliza awamu ya kwanza siku 20 kabla ya muda uliopangwa kwenye mkataba.
Mwinjuma alimaalufu kama Mwana Fa amesema: “Mkataba huu wa ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo jijini Arusha, ulitiwa saini tarehe 19, mwezi wa 3, mwaka jana (2024), lakini natambua kazi rasmi zilianza tarehe 25, mwezi wa 7, mwaka huo huo, baada ya utaratibu wa kukabidhiana site pamoja na shughuli zingine za awali kukamilika. Mkandarasi amepewa jukumu la kufanya usanifu, kujenga, na kufanya manunuzi muhimu yatakayokamilisha usanifu wa mradi huu kwa kuzingatia vigezo elekezi.”
Aliongezea, “Hivyo, tangu mradi kuanza, mkandarasi ulijielekeza kuanza kazi zako katika maeneo hayo mara moja kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi wa Wizara, Dar Al-Handasah, ili kutekeleza majukumu yako ya kikimkataba. Kwa kumbukumbu nilizonazo, kazi hii kwa upande wa ujenzi katika saite, hususan umwagaji wa zege, ulianza kutekelezwa tarehe 25, mwezi wa 11, mwaka 2024. .Leo hii, tarehe 19, mwezi wa 7, mwaka 2025, ikiwa ni siku 236 baadaye, shughuli kubwa ya kumwaga zege takribani mita za ujazo elfu 50 inakamilika. Hii inadhihirisha umakini, weledi, na ustadi wa hali ya juu wa Mkandarasi.”
Naibu Waziri aliendelea kusema kuwa kazi hiyo iliyotukuka ya mkandalasi inawapa tumaini kubwa Serikali na watekelezaji wa mradi huo, kuwa kazi itakamilika kwa wakati na kwa viwango tunavyotarajia.
“Kwa kasi hii mliyoionyesha, Watanzania wana uhakika wa kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON mwaka 2027, nasi tunajivunia kusimama mbele yao tukiwadhihirishia, kwa vitendo, kuwa shauku yao itatimia. Mradi unatazamiwa kukamilika tarehe 24 mwezi wa 7 mwaka kesho, na tunaamini hilo linawezekana. Hii itatuwezesha kuutumia uwanja, kuujua na kujiandaa vizuri kabla ya mashindano ya AFCON.”
Mwana Fa alieleza kuwa, mafanikio na kasi ya CRCEG mpaka kufikia hatua hii ni kutokana na ushirikiano ambao kwanza Serikali, kupitia Wizara yake ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, unauonyesha kwa kufanya malipo kwa wakati na kutoa ushirikiano katika vyombo vingine mbalimbali vya kiserikali vinavyosimamia shughuli hii pale unapohitajika.
“Aidha, kwa kurahisisha shughuli za Mkandarasi za kitaalamu na usimamizi, natambua mchango mkubwa unaowekezwa katika utekelezaji wa mradi kupitia Mshauri Elekezi, Dar Al-Handasah, pamoja na Ofisi ya Msimamizi wa Wizara iliyopo hapa hapa site, yaani Clerk of Work. Vile vile tunatambua kuwa kuwepo kwa ofisi hizi katika mradi kunasaidia kuzitatua changamoto kwa wakati pindi zinapojitokeza, lakini pia kurahisisha utekelezaji na kusababisha Mkandarasi kujielekeza mojakwa moja katika utekelezaji wa mradi, ” alisema Naibu Waziri na kusisitiza.
“Ushirikiano huu unazidi kujenga mahusiano yetu, kati ya mtu mmoja mmoja, makampuni ya kichina na ya wazawa kupitia mikataba midogo, wafanyabiashara na wataalamu wa ndanii inasaidia kuhamisha ujuzi na kubakiza ufanisi nchini, na pia inazidi kuimarisha mahusiano kati ya Serikali ya Tanzania na China..”
Mwana Fa ambaye pia ni Mbunge wa Muheza alisema kuwa mradi huo ni mmoja wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. “Pongezi na asante nyingi zimfikie, anapoona juhudi hizi bila shaka zinamtia moyo na kuzidi kumuhakikishia kuwa thamani ya pesa na maono ya Serikali yake yana tija na kuwapa tumaini watanzania.”
Alimalizia kwa kusema kuwa mradi huo ni wa kimkakati, unaodhamiria kuongeza chachu ya michezo nchini, ikiwa ni jitihada za makusudi kulea vipaji na kutengeneza jamii yenye nguvu na afya borakupitia michezo.
“Niwatie moyo wakandarasi na wadau wote wanaohusika katika utekelezaji wa mradi huu; historia inajengwa, na tunayo kila sababu ya kujivunia kuwa miongoni mwa watekelezaji. Mradi huu ukaweke alama nyingine kubwa katika uhusiano kati ya Tanzania na China.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi amesema: “imekuwa nikiufuatilia kwa ukaribu sana mradi huu wa ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo jijini Arusha tangu ulipoanza kutekelezwa mwaka jana(2024). Sababu ya kuufuatilia mradi huu kwa ukaribu huo ni kutokana na kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 338 za Kitanzania zinawekezwa katika utekelezaji wa mradi huu.”
RC aliongezea: “Lakini pia, mimi ni mdaumkubwa wa michezo, nikiamini kuwa michezo ni nguzo mojawapo ya kuimarisha afya na nguvu kwa vijana ambao ni taifa la kesho, na kwa Watanzania wote kwa ujumla.”
Amesema kuwa anatambua kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 24 mwezi wa saba mwaka kesho. “, Mimi, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu, nafurahishwa na juhudi zinazofanywa na mkandarasi katika utekelezaji wa mradi.
Kwa kasi ninayoiona, ni wazi kuwa mradi utakamilika ndani ya wakati, ili wakazi wa Arusha wawe wa kwanza kuutumia uwanja huu na kuonajuhudi inayofanywa na serikali yao,si kwa maneno tu bali kwa vitendo.”
Aliongezea kuwa Arusha ni kitovu cha utalii, na uwanja huu ni kivutio kingine cha utalii wa michezo.
“Hivyo, naendelea kuwaasa wakandarasi na wadau wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kujituma ili kukamilisha mradi kama inavyotarajiwa. Kiuchumi, natambua jinsi ambavyo shughuli za ujenzi wa uwanja huu umetengeneza ajira kwa vijana na wanawake wengi,” alisema.
RC Kihongosi alisistiza; “Lakini pia, utakapokamilika, uwanja huu utazalisha ajira zaidi, kuibua biashara mpya zinazohusiana na michezo na burudani, kukuza sekta ya utalii, na kuchangia katika pato la taifakwa ujumla. Kwa hiyo, kwangu mradi huu ni wa muhimu sana, na nausubiria kwa hamu kubwa.”
Aliwaeleza wakandarasi wanatekeleza mradi huo kuwa atendelea kuwapa ushirikiano katika masuala yote ya kiutawala, utaratibu, vigezo, na usimamizi unaotarajiwa kutolewa na ofisi yangu pamoja na taasisi zilizo chini yake ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mafanikio na viwango.
“Aidha, nitoe rai kwa wadau wote wa utekelezaji wa mradi huu kusimamia kwa umakini, kwa uadilifu, na kwa uwajibikaji mkubwa fedha na muda wa utekelezaji, ili thamani ya fedha ionekane na maono ya Serikali yatimie. Mafanikio ya mradi huu yatakuwa sababu nyingine ya kuendeleza mahusiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China, ” alisema.
Vilevile, amesema kuwa mradi huo umefungua fursa za kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo baina ya wataalamu na wakandarasi wa ndani, katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa maslahi ya Taifa la leo na la vizazi vijavyo.
Alimalizia kwa kusema: “Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha itaendelea kutoa ushirikiano wake kikamilifu ili kuhakikisha maandalizi ya mashindano ya AFCON yanafanyika kama yanavyotarajiwa, na kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya nchi yetu.
“Kwa dhati kabisa, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara na wa kizalendo wa kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo nchini,ikiwa ni sehemu ya kukuza vipaji, kuimarisha afya za Watanzania, na kulinda heshima ya nchi kimataifa.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya CRCEG Wang Yusheng amesema: “Kwa niaba ya CRCEG, napenda kutoa shukrani kubwa kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na serikali ya Tanzania kwa ukarimu, upendo, na msaada wao wakati wote tangu kuanza kwa mradi. Pia, nawashukuru vyema washauri elekezi, na timu zote zilizoshiriki katika ujenzi huu mpaka kufikia hapa. Zaidi ya hayo, ninawapongeza wafanyakazi wote waliojitoa usiku na mchana kwenye mradi huu mpaka kupelekea kazi hii kufikia hapa, tunawashukuru sana.”
Yusheng aliongezea: ” Tangu kuanza kwa ujenzi wa Uwanja huu wa Michezo mnamo tarehe 25 Julai 2024, chini ya uangalizi wa viongozi wetu na msaada wa wadau mbalimbali, tumeshinda changamoto nyingi. Kwa bidii ndani ya siku 360, tumefanikiwa kumaliza kazi ya zege kwa siku ishirini kabla, na haya ni mafanikio makubwa ya awali.”
Amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo ni mfano mzuri katika kuonyesha ushirikiano wa nchi ya China na Tanzania, na uthibitisho wa jitihada za CRCEG katika kuijenga “Mpango wa Mkanda Moja na Njia Moja”. Hii ni kuhakikisha uwanja unakamilika kwa ubora. Uwanja huu utakuwa jukwaa jipya la michezo wa mpira wa miguu, likisaidia Tanzania kukua kimichezo, kuboresha sura ya jiji, na kuvuta fursa za maendeleo. Pia kuleta mchango mpya kwenye uchumi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
“Tunatambua kuwa hii ni hatua moja, lakini bado kuna hatua nyingine zaidi ili kukamilisha mradi huu. Hatua hii ya mwanzo ni mwendelezo wa jitihada mbalimbali ambazo tayari tumezianzisha. Huu ni ushaidi wa dhamira yetu ya kusonga mbele ili kufanikisha malengo ya mradi huu. Kwa dhima ya “Uhuru, Umoja na Kazi” ya Reli ya TAZARA, tutaendelea kufanya kazi kwa bidii, kupanua mipango, na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati mnamo Julai 2026.
“Mwisho, Nawatakia kila la kheri, katika majukumu yenu ya kujenga Taifa, na tunatarajia uwanja huu kukamilika ili utumike kama ilivyopangwa. Hii itachochea kuimarika kwa urafiki kati ya nchi ya China na Tanzania mara dufu. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Naibu waziri na wageni wote, nawatakia Afya njema na mafanikio makubwa.Asante”.