Na MwandishiWetu, Dodoma
Katika kuhakikisha Vijana Mkoani Mara wanashiriki katika mnyororo wa thamani wa madini, Mkoa huo kwa kushirikiana na Tume ya Madini na Mgodi wa Barrick North Mara umewezesha upatikanaji wa lesseni 104 kwa vikundi 48 vyenye jumla ya Vijana 1,836 kutoka Vijiji 13 katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
Hayo yameelezwa leo Julai 18,2025 hapa Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi, wakati akizungumza na Watanzania kupitia mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika mkoa huo.
“Uwezeshaji wa makundi hayo ni semehu ya utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) na una lengo la kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini,”amesema.
Amesema Vijana hao wanapatiwa elimu kuhusu uchimbaji wa madini chini ya uangalizi wa Mgodi wa Barrick North Mara, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Ofisi ya Madini Mkoa.
Katika hatua nyingine Kanali Mtambi amesema hadi kufikia Juni 30, 2025, shilingi trilioni 1.3 zimetolewa na Mhe. Rais kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mara.
“Miradi iliyotekelezwa imesaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, kujifunzia, kuboresha miundombinu ya sekta mbalimbali na kuimarisha biashara,”amesema.
Aidha akigusia katika sekta ya Afya amesema Mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya ni pamoja na kuongezeka kwa Vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka vituo 321 mwaka 2020 hadi 421 mwaka 2025.
“Kliniki zimeongezeka kutoka 4 hadi 11, zahanati kutoka 263 hadi 333, Vituo vya Afya kutoka 42 hadi 56, Hospitali kutoka 11 hadi 20, Hospitali za Halmashauri kutoka tatu hadi 11. Idadi ya Nyumba za Watumishi imeongezeka kutoka nyumba 221 mwaka 2020 hadi 286 mwaka 2025. Idadi ya Watumishi wa Afya imeongezeka kutoka 2,515 mwaka 2020 hadi 3,644 mwaka 2025,”amesema.
Katika sekta ya Maji Mkoa wa Mara umefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 54 mwaka 2021 hadi asilimia 81 Juni, 2025.
“Upatikanaji wa maji safi na salama katika miji unaridhisha na hadi kufikia Juni, 2025 upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Musoma ni asilimia 98, Mji wa Mugumu asilimia 67, Mji wa Tarime asilimia 77 na Mji wa Bunda ni asilimia 86,”amesema.
Mkoa wa Mara una Wilaya sita za Musoma, Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya zenye Halmashauri tisa na majimbo 10 ya uchaguzi. Mkoa una Tarafa 20, Kata 178, Vijiji 458, Mitaa 242 na vitongoji 2,502.
Ambapo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mkoa wa Mara una watu 2,372,015 (wanawake 1,232,504, wanaume 1,139,511) na ongezeko la watu ni asilimia 3.1 kwa mwaka.