Featured Kitaifa

MADEREVA 42 WAFUNGIWA LESENI MBEYA.

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Fraisser Kashai kutoka Kamisheni ya Oparesheni na Mafunzo amewataka madereva wa mabasi ya abiria kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Ameyasema hayo Julai 18, 2025 baada ya kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria kabla ya kuanza safari katika stendi kuu Jijini Mbeya na kuwataka madereva kutii sheria za usalama barabarani na kwa yeyote atakayebainika kukiuka Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoani humo limeendelea kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwafungia leseni za udereva miezi mitatu na kwamba kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2025 jumla ya madereva 42 wamefungiwa leseni.

SSP Notker ametaja baadhi ya makosa hatarishi yaliyopelekea madereva kufungiwa leseni ni pamoja na mwendo kasi, kuyapita magari mengine katika maeneo yasiyoruhusiwa na ulevi na kuwataka madereva kutii sheria kwani Jeshi la Polisi halitakuwa na muhari kwa dereva yeyote atakayekamatwa kwa makosa hatarishi.

Naye, Afisa Mfawidhi LATRA Mkoa wa Mbeya Shaban Mdende amesema kuwa mabasi ya abiria yamefungwa kifaa maalum cha mwenendo ambapo LATRA na Jeshi wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano na Kufuatilia mwenendo wa mabasi kupitia mfumo wa VTS ambapo kati ya madereva 42 waliofungiwa leseni, madereva 26 ni baada ya kuwabaini kupitia mfumo wa VTS.

Ukaguzi uliofanywa na DCP Kashai umehusisha ukaguzi wa magari, leseni za udereva, kupima kilevi madereva na utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa abiria huku lengo likiwa ni kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na kutoa elimu kwa madereva na abiria ili kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

About the author

mzalendoeditor