Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa (Kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – (TASAF), Ndg. Japhet Boaz,wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyozinduliwa leo Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Na Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shedrack Mziray amesema uzinduzi wa Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) si tukio la kisiasa tu bali ni hatua ya kimkakati inayoashiria safari ya pamoja kuelekea Tanzania yenye uchumi jumuishi na ustawi wa wote.
Akizungumza mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuizindua rasmi Dira hiyo jijini Dodoma, Mziray amesema mpango huo wa muda mrefu unakuja wakati nchi iko kwenye hatua ya uchumi wa kati daraja la chini na inalenga kufikia uchumi wa kati daraja la juu ifikapo 2050, kwa kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma.
“Uchumi huu unaotarajiwa ni uchumi jumuishi ambapo wananchi wote wanufaike. Maendeleo ya kiuchumi hayawezi kuwa kamilifu bila ustawi wa jamii. Ndiyo maana shughuli za TASAF zinaendana moja kwa moja na malengo ya Dira hii mpya,” alisema Mziray.
Alisema TASAF imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu kupitia miradi ya hifadhi ya jamii, kwa kutoa ruzuku kwa kaya maskini, kusaidia mahitaji ya msingi kama elimu na afya, na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi.
Aidha, amesema kuwa Dira ya 2050 imeweka bayana umuhimu wa kuhakikisha watu wa hali ya chini wanaunganishwa na fursa rasmi za maendeleo, na kwamba ni lazima afua za kijamii ziwafikie walengwa kwa usahihi.
Amesema hiyo ndiyo sababu Serikali kupitia TASAF inatambua kuwa asilimia 26 ya Watanzania bado wanaishi kwenye mazingira ya umaskini wa hali ya chini.
“Ni muhimu sana kuhakikisha watu hawa wanakuwa sehemu ya mchakato wa maendeleo. Mfano kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote tunawawezesha wananchi kupata huduma bora za afya bila mzigo wa gharama.
Hivyo hivyo kwa elimu watoto wa kaya maskini wanawezeshwa kwenda shule, kupata vifaa, sare na mazingira bora ya kujifunza,” alifafanua Mziray.
Alisisitiza kuwa mchango wa TASAF utabaki kuwa mhimili katika kufanikisha maendeleo ya pamoja, lakini alitoa wito kwa wananchi wote kuiisoma, kuielewa na kuitafsiri Dira ya 2050 kwa vitendo, akisema haitoshi kuipokea kwa shangwe, bali ni lazima kila mmoja atambue nafasi yake na kushiriki moja kwa moja.
“Tusiwe watazamaji. Tuitikise jamii zetu, tushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira hii. Hii si ndoto ya Serikali peke yake, ni ndoto ya Watanzania wote. Tuifanye kuwa ya kweli,” alisema kwa msisitizo.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – (TASAF), Ndg. Japhet Boaz , amesema hatua ya kuzinduliwa kwa Dira hiyo ni uthibitisho kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imejiandaa kikamilifu kuelekea miaka 25 ya kupanga kwa ufanisi maendeleo jumuishi kwa makundi yote ya wananchi.
Amesema tayari ameisoma Dira hiyo kwa kina na kujipanga kushiriki katika eneo la kusaidia kaya maskini, wazee, na jamii zilizoathiriwa na majanga kupitia mipango ya hifadhi ya jamii, elimu, na bima ya afya kwa wote.
Amesema Dira hiyo imeweka msingi madhubuti wa kujenga taifa lenye usawa na mshikamano kwa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.
“Serikali imeandaa mpango jumuishi na sisi kama taasisi tumejipanga kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi unaogusa watu wa kawaida. Kwa kasi ya sasa na malengo yaliyowekwa, ninaamini mwaka 2050 Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya hapa tulipo, si kiuchumi tu bali hata katika ustawi wa jamii,” alieleza.
Boaz aliongeza kuwa Mpango mkakati wa utekelezaji wa Dira 2050 umegawanywa katika vipindi vya utekelezaji wa miaka mitano mitano, jambo linalowezesha kuwekwa kwa vipaumbele na tathmini ya utekelezaji kwa kila hatua. Alisisitiza kuwa Dira hiyo ni mpango makini ambao unaweza kabisa kubadilisha maisha ya Mtanzania wa kawaida, endapo kila mdau atashiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wake.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shedrack Mziray (Kulia) akisalimiana na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa (Kushoto) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyozinduliwa leo Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa (Kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – (TASAF), Ndg. Japhet Boaz,wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyozinduliwa leo Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shedrack Mziray (Kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – (TASAF), Ndg. Japhet Boaz (Kulia) ,wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iliyozinduliwa leo Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. Shedrack Mziray (Katikati) akiwa na Mkurugenzi Mifumo, Tafiti na Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – (TASAF), Ndg. Japhet Boaz (Kulia) wakionesha Vitabu vya Muongozo wa Dira 205o,mara baada ya Dira hiyo kuzinduliwa leo Julai 17,2025 jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.