MKUU wa Mkoa wa Mwanza Bw.Said Mtanda ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 16,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Bw.Said Mtanda ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 16,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Bw.Said Mtanda ,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 16,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025.
Alex Sonna_ Dodoma
SERIKALI Mkoani Mwanza imesema inaendelea kuweka mikakati kabambe ya kudhibiti na kusimamia ipasavyo ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini kiholela katika Wilaya ya Misungwi, hususan maeneo ya Busongo, Kasadi na Ishokela Hela.
Hayo yameelezwa leo Julai 16,2025 Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw.Said Mtanda wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita kwenye Mkoa huo na kusisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi kwa njia rasmi, salama na endelevu.
Akizungumzia hali ilivyo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza amesema kuwa mkoa huo kwa sasa unaibuka kwa kasi katika sekta ya madini na hivyo unahitaji usimamizi madhubuti na wa karibu ili kuondoa mianya ya uchimbaji usio rasmi, usio na tija wala usalama kwa wachimbaji na mazingira.
Amesema, “Mkoa wa Mwanza umejaaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini, na hiyo ndiyo sababu maeneo kama Busongo,Kasandi,Ishokela Hela na maeneo mengine yaliyopo wilayani Misungwi yamekuwa kivutio kikubwa kwa wachimbaji,
Tunatambua kuwa kuna uchimbaji holela na ndiyo maana tumechukua hatua madhubuti kuhakikisha wachimbaji wanafanya shughuli zao kwa kufuata sheria, huku wakiwa salama na wakinufaika kiuchumi,” amesema RC Mtanda.
Amebainisha kuwa tayari Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Madini wa Mkoa (RMO) imeanza kazi ya kwenda moja kwa moja kwenye maeneo husika, kuwatambua wachimbaji, kuwaunganisha kwenye vikundi rasmi, kuwapa elimu ya kitaalam kuhusu mbinu bora za uchimbaji, na kuwaandikisha ili waweze kusajiliwa kisheria.
“Tunataka kila mchimbaji awe sehemu ya mfumo rasmi, Kwa sasa tunafanya utambuzi katika maeneo yote yenye dalili za uchimbaji, na tumewapa wachimbaji elimu ya namna ya kuchimba kisasa, salama na kwa kuzingatia sheria,”ameeleza Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza na kueleza;
Mchimbaji aliyesajiliwa anakuwa na nafasi ya kupata msaada wa kitaalam, mikopo na hata masoko ya uhakika,hii itawasaidia wao kuongeza kipato na kuwa na uhalali wa kufanya shughuli zao kwa Uhuru, ” ameeleza Mtanda
Kwa mujibu wa Mtanda, maeneo mengi yaliyokuwa na uchimbaji wa kiholela sasa yameanza kubadilika kutokana na juhudi hizo, huku serikali ikisisitiza kuwa pale yanapojitokeza makundi yanayojihusisha na uchimbaji haramu, hupelekwa timu maalum ya ufuatiliaji inayojulikana kama RUSH (Rapid Unit for Safety and Harmony) kushughulikia kwa haraka.
Mbali na juhudi hizo, Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza unatarajia kwa matumaini makubwa kuanza kwa shughuli za mgodi mkubwa wa kimataifa wa Nyanzaga, ambao unaelezwa kuwa utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mkoa, kutoa ajira kwa wananchi wa maeneo ya jirani, na kuinua biashara ndogondogo zinazozunguka mgodi huo.
“Kauli mbiu ya Madini inasema ‘Madini ni Utajiri’ na tunataka wananchi wetu waishi kwenye rasilimali zao kwa mafanikio, lengo letu ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanabadilika kuwa wajasiriamali wakubwa kupitia elimu, usimamizi bora na sera madhubuti za sekta ya madini,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa kwa sasa, Serikali ya Mkoa inaendelea kusimamia kwa karibu shughuli zote zinazohusiana na madini katika Wilaya ya Misungwi na maeneo mengine ya Mkoa wa Mwanza, huku ikishirikiana na wizara husika kuhakikisha kila rasilimali inatumiwa kwa manufaa ya Taifa na wananchi walioko karibu na migodi.
RC Mtanda, amesema kuwa serikali imejidhatiti kikamilifu katika kuhakikisha kuwa changamoto ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Misungwi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu hususani barabara ya Mwanangwa,Misasi,Busongo na barabara ya Buhingo kwenda Mbarika
“Tumejipanga kuhakikisha barabara zote muhimu kwa uchumi wa wananchi, hasa zile zinazotumika kusafirisha mazao na bidhaa za kibiashara, zinaboreshwa. Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya barabara,”amesema RC Mtanda
Ameongeza kuwa tayari baadhi ya barabara zimeanza kufanyiwa ukarabati, huku nyingine zikiwa kwenye hatua ya upembuzi yakinifu kabla ya kuanza kwa ujenzi. Aidha, alisisitiza ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kutunza miundombinu hiyo mara baada ya kukamilika.
Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango vinavyodumu kwa muda mrefu, na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya na mkoa kwa ujumla.