Kitaifa Michezo

NM-AIST YAZINDUA JEZI RASMI KWA MBIO ZA NELSON MANDELA,WAKIMBIAJI WA KIMATAIFA KUWASHA MOTO ARUSHA

Written by mzalendoeditor

 

Makamu Mkuu wa Taasisi Prof Maulilio Kipanyula (katikati) pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ubunifu Prof Anthony Mshandete (kushoto) na Meneja Biashara kutoka Benki ya CRDB Mbelwa Luhambiga (kulia) wakionyesha T-shirt, Namba na medal ikiwa ishara ya uzinduzi wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili ambazo zitakazofanyika Julai 20,2025 ambapo Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi

……

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imezindua rasmi jezi za msimu wa pili wa Mbio za Nelson Mandela, zenye kauli mbiu “Jitihada kwa Sayansi, Hatua kwa Mafanikio,” tukio linalotarajiwa kufanyika kwa kishindo mnamo Julai 20, 2025 katika Kampasi ya taasisi jijini Arusha.

Katika uzinduzi huo leo Julai 15,2025, Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa, Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha mbio hizo.

“Mbio hizi si za kawaida tu; ni sehemu ya harakati za kuhamasisha elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kwa vitendo. Tunaamini kwamba kupitia michezo, hasa riadha, tunaweza kufikia jamii kwa urahisi zaidi na kuvutia vijana, hasa wasichana, kujiamini na kushiriki katika taaluma za kisayansi,” alisema Prof. Kipanyula.

Aidha, Prof. Maulilio amesema mwaka huu mbio zitavutia zaidi kutokana na ushiriki wa wakimbiaji wa kimataifa kutoka nje ya nchi, pamoja na mbio maalum za watoto wa kilomita 2.05 zitakazoweka historia mpya ya ushirikishwaji wa kizazi kipya.

Mbio hizo zinahusisha Kilomita 2.05 kwa ajili ya watoto, Kilomita 5, Kilomita 10 na Nusu Marathon (KM 21), na si tu kwa lengo la ushindi bali kama jukwaa la kuhamasisha jamii, hasa wasichana na wanawake vijana, kushiriki kikamilifu katika elimu ya STEM kupitia michezo. Amesisitiza.

Meneja wa Biashara wa Benki ya CRDB, Mbelwa Henry Luhambiga, ambaye benki yake ni miongoni mwa wadhamini wakuu wa mbio hizo, amesema:

“Michezo ni chachu ya maendeleo ya jamii. Kupitia Mbio za Nelson Mandela, tunawawezesha watu kuimarisha afya zao huku tukijenga mshikamano wa kijamii na kukuza vipaji. CRDB inajivunia kuwa sehemu ya harakati hizi za kijamii zenye mwelekeo wa kitaaluma na kiafya.”

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha, John Steven, amesema kuwa:

“Mbio za mwaka huu zitashirikisha wakimbiaji wa kimataifa wanaojiandaa kwa mashindano ya Dunia ya Riadha yatakayofanyika Tokyo, Japan, Septemba 13, 2025. Hii ni fursa muhimu kwa wakimbiaji wa ndani kujifunza na kujitangaza kimataifa.”

Taasisi pia imewashukuru wadhamini wote walioungana kwa msimu huu wa pili, wakiwemo Coca-Cola Bonite Bottlers Ltd, CRDB Bank, Kilimanjaro Drinking Water, NSK Hospitals, Tanzania Red Cross Society, pamoja na wadau wengine wa afya, usalama na michezo.

“Huu si mwendo wa kawaida – ni mbio za kuandika historia, kuchochea elimu, na kuibua vipaji vya kesho,” alisema Prof. Kipanyula.

Amewataka wananchi wote kujitokeza na kushiriki mbio hizo kubwa, kuvaa jezi rasmi kwa fahari, na kuwa sehemu ya safari ya mabadiliko kutoka darasani hadi viwanjani.

Makamu Mkuu wa Taasisi Prof Maulilio Kipanyula (katikati) pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ubunifu Prof Anthony Mshandete (kushoto) na Meneja Biashara kutoka Benki ya CRDB Mbelwa Luhambiga (kulia) wakionyesha T-shirt, Namba na medal ikiwa ishara ya uzinduzi wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili ambazo zitakazofanyika Julai 20,2025 ambapo Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi.

Makamu Mkuu wa Taasisi Prof Maulilio Kipanyula (kushoto)akimkabidhi Tshirt na namba ya ushiriki wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili Meneja Biashara kutoka Benki ya CRDB Mbelwa Luhambiga (kulia) ambao ni mojawapo ya wadhamininwa mbio hizo wakati wa uzinduzi wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili zitakazofanyika Julai 20,2025 ambapo Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi.

Makamu Mkuu wa Taasisi Prof Maulilio Kipanyula (kushoto)akimkabidhi Tshirt na namba ya ushiriki wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili Mwakilishi kutoka Cocacola Bonite Bottlers Ltd Bi. Philipina (kulia) ambao ni moja ya wadhamini wa mbio hizo wakati wa uzinduzi wa Nelson Mandela Marathon msimu wa pili zitakazofanyika Julai 20,2025 ambapo Mgeni Rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Mwinyi Ahmed Mwinyi.

Kamati ya Maandalizi ya Nelson Mandela Marathon msimu wa pili wakiwa wamevalia t-shirt rasmi za msimu wapili tayari kwa mbio hizo Julai 20,2025 jijini Arusha.

Muonekano wa Medali na t-shirt za mbio za Nelson Mandela (Marathon) msimu wa pili zitakazofanyika Julai 20,2025.

About the author

mzalendoeditor